Wananchi wameaswa kuendelea kuchangia damu sehemu mbali za mkoa wa Dar es salam ili kuwasaidia watu wenye uhitaji
Hayo yameeoezwa na mganga mkuu wa mkoa wa Dar es salam Dkt. Rashid Mfaume alipokuwa anaongea na wanahabari katika Bonanza la uchangiaji damu salama lililofanyika jana Wazo Mivumoni wilayani Kinondoni
Akiendelea kutoa hamasa kushiriki zoezi la uchangiaji damu salama Dkt. Mfaume amesema anawahamasisha wananchi kushiriki katika kampeni mbalimbali za uchangiaji wa damu salama katika mitaa, Wilaya na hospitali mbali mbali zilizopo jirani na maeneo yao ili kuwasaidia wenye uhitaji.
Zoezi la uchangiaji damu salama Wazo Mivumoni limeandaliwa na kuratibiwa na Anjela Seth mwandishi wa habari kutoka fullshangweblog ambapo Anjela amesema dhumuni kubwa la kuandaa Bonanza hilo ni kutoa hamasa kwa waandishi wenzake pamoja na wananchi kujitokeza kuhamasisha uchangiaji wa damu salama mara kwa mara.
Aidha mganga mkuu wa mkoa wa DSM ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mratibu wa Bonanza hilo pamoja na mchungaji Richard Hananja ambaye ni mlezi na kuwasihi watu wengine kujitokeza kuandaa mabonanza na matamasha ya uchangiaji wa damu salama kwani kwa sasa uhitaji ni mkubwa sana.
Kwa upande wake mchungaji Richard Hananja amasema anawashukuru wote waliojitokeza kwenye zoezi hilo na kuwaomba kuwa na moyo wa kusaidia wengine kwani kuchangia damu ni sadaka kubwa ambayo haina mfano.
Naye Joyce Joseph Mnasihi kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili amesema anawashukuru waandaaji wa zoezi hilo pamoja na wananchi wote waliojitokeza kuchangia damu ili kuweza kuokoa maisha ya wenye uhitaji na kusema hospitali ya Taifa Muhimbili kwa sasa ina uhitaji mkubwa sana wa damu wakiwemo watoto chini ya miaka mitano, wakina mama wanaojifungua, watu wenye Kansa pamoja na wagonjwa mbalimbali.