Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Mussa Haji Mussa akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar,umempongeza Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt.Hussein Mwinyi, kwa kutoa hotuba yenye muelekeo wa kuimarisha Uchumi,Siasa na masuala ya kijamii ndani ya Chama na Jumuiya zake.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Mussa Haji Mussa,mara baada ya kukamilika kwa ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Dk.Mwinyi,iliyofanyika Mkoa wa Magharib Kichama huko Wilaya ya Magharib ‘B’ Unguja.
Alisema hotuba iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi,imeongeza imani na matumaini kwa Wanachama na makada wa CCM hasa Vijana.
Naibu Mussa,alieleza kwamba Rais Dk.Mwinyi ,amekuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa katika kupigania maslahi na haki kuimarisha maendeleo ya Nchi.
Alisema katika hotuba ya leo Dk.Mwinyi,alionyesha dhamira ya kuimarisha Chama kwa kutumia rasilimali zilizopo kujiimarisha kiuchumi kwa kutatua changamoto za majengo chakavu na kuimarisha maslahi ya Watumishi wa CCM.
Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo Mussa,alifafanua kuwa kiongozi huyo amekemea migogoro inayosadikiwa kutengeneza na Viongozi wa majimbo ambapo amewataka kuacha tabia hizo na kuwa wamoja.
Mussa,aliweka alifafanua kuwa Dkt.Mwinyi, aliwasihi Viongozi wa Chama na Serikali kujua kuwa Mkataba wa CCM na Wananchi ni Ilani ya Uchaguzi hivyo Viongozi na Watendaji waliopewa dhamana ya kuwakilisha Wananchi watekeleze ahadi zao kwa ufanisi.
“Nasaha zangu kwa Vijana wenzangu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla tuendelee kumuunga mkono Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi,kwa Kasi yake ya utendaji ili aweze kufikia malengo ya kufanya Mapinduzi makubwa ya kiuchumi nchini”,alisema Naibu Katibu Mkuu huyo Mussa.
Pamoja na hayo alisema UVCCM utaendelea kuwa chachu na chimbuko la Vijana wazalendo wenye imani na utii wa kulinda na kutetea maslahi ya CCM popote ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa nchi yenye amani na utulivu wa kudumu.