Na Victor Makinda. Igunga.
Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Igunga Mkoani
Tabora, kimesema juhudi za Rais wa awamu ya sita wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu
Hassan, zinatoa muelekeo chanya wa ukuaji wa sekta ya
elimu nchini.
Hayo yameelezwa na Katibu wa CWT Wilayani Igunga
,Sophia Maziku, alipozungumza na mwandishi wetu
ofisini kwake mjini Igunga mapema leo.
Maziku amesema kuwa, uwekezaji mkubwa unaofanywa
na serikali ya awamu ya sita katika sekta ya Elimu nchini
unaleta tija na ufanisi kwenye ukuaji wa sekta hiyo
muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
"Kwa niaba ya Walimu wilayani Igunga kwanza
tunampongeza sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi
ambavyo Serikali yake inavyotatua changamoto za elimu
kwa kujenga madarasa, nyumba za Walimu sambamba na
kuboresha maslahi ya walimu kote nchini." alisema
Maziku.
Aliongeza kusema kuwa, Hatua ya Serikali kulipa
malimbikizo ya madeni ya Walimu, kupandisha madaraja
pamoja na kuanza kuorejesha utaratibu wa nyongeza ya
mishahara kila mwaka imeongeza ari na mori ya Walimu
kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
" Ahadi ya Rais Dkt Samia siku ya maadhimisho ya siku
ya wafanyakazi duniani Mei Mosi, ya kwamba
wafanyakazi kote nchini mambo yao yatakuwa moto
kuanzia bajeti ya 2023/2024 itakayo anza kutekelezwa
mwezi Julai mwaka huu imewapa tabasamu wafanyakazi
wote hususani walimu wa wilaya ya Igunga," alisema
Maziku.
Katika hatua nyingine CWT wilayani Igunga imeahidi kuwa
bega kwa bega na Rais Samia ambapo wamesema kuwa
watamuunga mkono kwa hali na mali ili aweze kumaliza
vipindi vyake viwili vya Uongozi.
"CWT Igunga tunamuhakikishia Rais Samia kuwa tupo
naye bega kwa bega, tutapambana kumsaidia kwa lolote
huku tukiendelea kubaki kuwa wafuasi watiifu kwa serikali
yake." alisema Maziku.