MJUMBE wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Haji Machano(kulia), akisoma taarifa ya kumpongeza Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi, kwa kupandisha pensheni ya Wazee nchini, Mwenyekiti wa Baraza hilo Bi.Khadija Jabir Mohamed(kushoto) wakati wakizungumza na waandishi wa habari huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.
……
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
BARAZA la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar, limeeleza kuridhishwa na kasi kubwa ya utendaji wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,kwa kuendeleza kwa vitendo azma na malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Kauli hiyo imetolewa na Mjumbe wa Baraza hilo Haji Machano Haji wakati akizungumza na waandishi wa habari huko Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui.
Haji, amesema kuwa wamepokea kwa furaha kubwa hatua mbalimbali za utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kimaendeleo katika nyanja za kijamii,kiuchumi na kisiasa zikiwa ni juhudi za kuwaenzi,kuwatunza na kuwathamini wazee hao.
Alisema Rais Dk.Mwinyi, amekuwa ni kiongozi mzalendo na mwenye imani na maono yanayoishi katika dhamira ya malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyotekelezwa na nia ya kuwakomboa kiuchumi na kifikra wananchi wa Visiwani humo.
Katika maelezo yake Mjumbe huyo Haji, alisema baraza hilo linampongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi, kwa kupandisha pencheni kwa wastaafu kwa asilimia 100 ambapo utaratibu huo mpya unatarajiwa kuanza mwezi julai mwaka 2023.
Alieleza kwamba maamuzi hayo yametangazwa katika kilele cha sherehe za maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani iliyofanyika kitaifa Zanzibar huko Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo Dk.Mwinyi aliahidi kupandisha pensheni kwa wastaafu wa kima cha chini kufikia shilingi 180,000/= kutoka 90,000/=.
Alieleza Mjumbe huyo kwamba katika maelezo ya Dk,Mwinyi, alisema Serikali itapandisha pensheni jamii kwa asilimia 150 kwa wazee kuanzia miaka 70 ambapo watapokea 50,000/= kutoka shilingi 20,000/= wanayopokea hivi sasa.
“Sisi wazee wa CCM Zanzibar tumepokea kwa furaha kubwa maamuzi ya Rais wetu mpendwa Dk.Hussein Mwinyi, kitendo alichokifanya ni cha utu na ungwana wa kuonyesha namna anavyotuthamini wazee wake.
Pia hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 ibara ya 214 inayoeleza kuwa Chama Cha Mapinduzi kinatambua umuhimu wa wazee katika Taifa letu, na kitaendelea kuwapatia huduma za kijamii na kisheria na kwamba Chama,kimeielekeza Serikali katika kipindi cha miaka mitano(5) kuongeza bajeti ya mpango wa pensheni ya wazee kutoka bilioni 6.5 hadi shilingi bilioni 7 kwa malipo ya wazee wa Unguja na Pemba”,alifafanua Mzee Haji.
Pamoja na hayo alieleza kuwa kwa niaba ya wazee wote nchini wanaonufaika na pensheni hiyo, wataendelea kumuombea duwa na kuunga mkono kwa vitendo juhudi zote za maendeleo zinazotekelezwa na Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi chini ya Serikali anayoiongoza ya awamu ya nane.