NA FARIDA MANGUBE.MOROGORO.
Wakazi wa Wilaya za Kilombero,Ulanga na Malinyi wapo mbioni kuondokana na adha ya kukosekana kwa umeme wa uhakika katika maeneo yao baada ya ujenzi wa kituo cha kupooza na kusambaza umeme kinachojengwa katika mji wa Ifakara kukamilika ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.
Mradi huo ambao ujenzi wake ulianza mwaka 2020 ulitarajiwa kukamilika mwezi Machi mwaka huu lakini ulishindwa kukamilika kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona na Vita inavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine na hivyo kupelekea vifaa kwa ajili ya ujenzi huo kuchelewa kufika nchini.
Akizungumza katika ziara ya Wabia wa maendeleo wa katika ujenzi wa mradi huo wakiongozwa na umoja wa Ulaya ambao wametoa shilingi bilioni 16 kati ya ishirini na mbili za mradi huo,Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini REA Mhandisi Hassan Saidy amesema mradi huo utakamilika kama ulivyopangwa.
Mhandisi Saidy amesema kuwa mradi umefikia asilimia 90 ya ujenzi wake na ulianza kujengwa Machi 2020 na kughalimu zaidi ya Bil.20 huku ukitarajiwa kukamilika Agoust 2023
”Mradi huu wa kupoza umeme Ifakara utawezesha kupatikana kwa umeme wa kutosha masaa yote kwa wilaya za Ulanga na Kilombero,kukomesha kukatika umeme mara kwa mara.”amesema Mhandisi Saidy.
Pia ameema kuwa mradi huo unatarajiwa kuhudumia Wananchi takriban Elfu moja wa wilaya za Kilombero, Ulanga, Malinyi na maeneo jirani ambapo takribani vijiji na vitongoji 15 kwa Wilaya ya Kilombero.
Kwa Upande wake Mwanyekiti wa Bodi ya REA Janeth Mbene amesema Bodi yake itasimamia kuhakikisha REA inatekeleza miradi yote kikamilifu na kusambaza umeme kwenye vijiji vyote ambavyo bado havijafikiwa na nishati ya umeme.
Francis Songela Meneja miradi Umoja wa Ulaya amesema wao kama wabia wameridhishwa na kazi zinazoendelea katika ujenzi wa mradi huo na kwamba kazi ilibaki ni ndogo hivyo wanaimani ifikapo mwezi Agoust mwaka huu mradi utakuwa umekamilika.