Mkuu wa wilaya ya Mbulu Komredi Kheri James,mapema leo amewaongoza viongozi na watumishi katika zoezi la kupokea vifaa tiba kwa ajili ya wodi ya Dharura na wodi ya wagonjwa Mahututi vilivyo tolewa na Serikali kwa ajili ya Hospitali ya mji wa Mbulu.
Akizungumza katika mapokezi hayo, Kheri James amempongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi makubwa yanayo fanywa na Serikali katika sekta ya afya ndani ya wilaya ya Mbulu.
Kheri James ameeleza mafanikio ya ujenzi wa vituo vya afya,zahanati na ujenzi wa wodi za wagonjwa Mahututi,wodi za dharura pamoja na kuweka vifaa tiba ni ishara ya dhamira ya wazi ya Mheshimiwa Rais ya kuweka msingi wa huduma bora na za uhakika kwa wananchi.
Akizungumzia vifaa vilivyo pokelewa Komredi Kheri James ameeleza kuwa ujio wa vifaa hivyo utaokoa maisha ya wagonjwa,utapunguza mzigo wa rufaa kwa Wananchi, Utarahisisha huduma kwa wananchi, Utawarahisishia wataalamu wetu wa afya utendaji wao kwa kuwa na vifaa vya uhakika na vya kutosha pia Kheri James ameeleza kuwa uwepo wa vifaa hivyo utawapunguzia gharama wananchi tofauti ilivyo kuwa mwanzo wakati vifaa hivyo havijapatikana.
Viongozi, watumishi na wananchi wa Mbulu kwapamoja wanaendelea kuishukuru Serikali kwa uamuzi wa kuleta vifaa hivi, na wana ahidi kushirikiana kuvitunza ili viwafae kwa ufanisi na kwa muda mrefu.
Zoezi la mapokezi ya vifaa hivyo limehudhuriwa na Kamati ya usalama ya wilaya, Mkurugenzi wa Halimashauri ya Mji,Mganga wa wilaya,pamoja na viongozi na watumishi wa idara ya afya.