Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Willbroad Mutafungwa akitoa maelekezo kwa Mfanyabiashara kuhusu muhimu wa kufunga aCCTV Camera katika duka lake.
…….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wafanyabiashara Mkoani Mwanza wametakiwa kufunga CCTV Camera kwenye maduka yao hatua itakayosaidia kupata msaada wa haraka wa kuwakamata waharifu.
Rai hiyo imetolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza Willbroad Mutafungwa alipokuwa kwenye ziara ya mguu kwa mguu na kikosi kazi cha Maasikari Polisi kwa lengo la kukagua maduka mbalimbali kama wamefunga Camera hizo.
“Disemba 2022 nilitoa maagizo kwenye vituo vya mafuta na wamiliki wa maduka kufunga Camera hizo ndio maana leo nimefanya ziara ili kuangalia kama agizo langu limetekelezwa hivyo jiwekeeni utaratibu mzuri katika maduka yenu kwa kufunga CCTV Camera ili kuweza kuwa na kumbukumbu za matukio yote yanayofanyika”, alisema Kamanda Mutafunga.
Mussa Feleji ni Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za mitaa ya mjini kati ambapo ziara hiyo ilifanyika amesema wanaendelea kushirikiana kwa ukaribu na wafanyabiashara hao ikiwemo kuwasisitiza kuweka walinzi ambao wanatambulika na mashirika mbalimbali ya ulinzi.
Nao baadhi ya wamiliki wa maduka wamelishukuru jeshi la polisi kwa namna wanavyozidi kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao huku wakimuahidi Kamanda Mutafungwa kuwa watafunga Camera hizo.