Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji watatu wastaafu walioagwa leo pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama hiyo walioshiriki katika sherehe ya kuagwa kitaaluma kwa Majaji wastaafu iliyofanyika leo tarehe 04 Mei, 2023 katika ukumbi namba moja (1) wa Mahakama Kuu Dar es Salaam. Majaji wastaafu walioagwa ni pamoja na Mhe. Beatrice Rhoda Mutungi (wa kwanza kushoto kwa Jaji Kiongozi), Mhe. Sekela Cyril Moshi (wa pili kushoto) na Mhe. John Mgetta (wa kwanza kushoto).
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (mwenye suti ya bluu), Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma (kulia) pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama na wageni waalikwa wakifuatilia sherehe ya kuagwa kitaaluma Majaji watatu wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt akizungumza jambo wakati wa sherehe ya kuwaaga kitaaluma Majaji watatu wastaafu wa Mahakama hiyo.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu walioshiriki katika sherehe hiyo.
Watumishi wa Mahakama pamoja na wageni waalikwa wakifuatilia kinachojiri katika sherehe ya kuagwa Majaji wastaafu watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Mmoja kati ya Majaji wastaafu watatu walioagwa leo tarehe 04 Mei, 2023,Mhe. Beatrice Rhoda Mutungi.
Mmoja kati ya Majaji wastaafu watatu walioagwa leo tarehe 04 Mei, 2023, Mhe. Sekela Cyril Moshi.
Mmoja kati ya Majaji wastaafu watatu walioagwa leo tarehe 04 Mei, 2023, Mhe. John Samwel Mgetta.
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wastaafu na baadhi ya Majaji wa Mahakama hiyo walioshiriki katika sherehe ya kuwaaga kitaaluma Majaji wastaafu. Wa tatu kushoto ni Jaji Mstaafu, Mhe. Beatrice Rhoda Mutungi, wa kwanza kushoto ni Jaji Mstaafu, Mhe. Sekela Cyril Moshi, wa pili kulia ni Jaji Mstaafu, Mhe. John Samwel Mgetta, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi Kazi maalum Masjala Kuu, Mhe. Moses Mzuna, wa tatu kulia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi na wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Mahakama walioshiriki katika hafla hiyo.
Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na ndugu wa Majaji wastaafu. (Picha na Innocent Kansha, Mahakama)
…..
Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani ameongoza sherehe ya kuwaaga kitaaluma Majaji watatu wastaafu wa Mahakama hiyo ambapo amesema kwamba, Mhimili huo utaendelea kusimamia haki katika utendaji kazi na kuwaomba wananchi kuendelea kuwa na imani na chombo hicho.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 04 Mei, 2023 mara baada ya kuhitimisha zoezi la kuongoza sherehe hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, Mhe. Siyani amesema kuwa ni wajibu wa Majaji na watumishi wote wa Mahakama kuhakikisha kwamba wanaendelea kujenga imani ya wananchi dhidi ya Mahakama.
“Wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi na Mahakama, hivyo niwakumbushe wananchi kuendelea kutumia Mahakama zote kuanzia ngazi ya Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani kwakuwa ndipo haki inapopatikana,” amesema Jaji Kiongozi.
Mhe. Siyani amesema kwamba, wananchi wanapokosa imani kwa Mahakama maana yake hawatatumia chombo hicho na hivyo kutakuwa na ongezeko la vitendo vya uhalifu vitakavyohatarisha amani ya nchi.
Akizungumzia kustaafu kwa Majaji hao ambao ni Mhe. Beatrice Rhoda Mutungi, Mhe. Sekela Cyril Moshi na Mhe. John Mgetta, Jaji Kiongozi amesema kuwa watakumbukwa kwa uzoefu na umahiri wao katika kuendesha gurudumu la utoaji haki nchini.
“Kustaafu kwa Majaji hawa waliokuwa na uzoefu wa kutosha ni dhahiri kuwa kumeacha pengo, hivyo nitoe rai kwa Majaji wanaobaki kuchukua mazuri yote ambayo yameachwa na Majaji hawa ili kuendelea kuwahudumia vema wananchi,” ameeleza Mhe. Siyani.
Wakizungumza katika sherehe hiyo ya kitaaluma, Majaji wastaafu walioagwa wametoa rai kwa watumishi wa Mahakama kuimarisha ushirikiano katika kazi, kutokuwa na upendeleo, kufanya kazi kwa bidii na kuendeleza matumizi ya TEHAMA.
Katika sherehe hiyo maalum ya kitaaluma Jaji Kiongozi aliongoza jopo lenye jumla ya Majaji 24 wa Mahakama Kuu na vilevile imehudhuriwa na pia baadhi ya watumishi na Viongozi wa Mahakama ambao ni pamoja na Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma. Kadhalika imehudhuriwa na ndugu, jamaa na marafiki wa Majaji wastaafu.
Wadau waliohudhuria katika sherehe hiyo ni pamoja na Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).
Zoezi la kuwaaga kitaaluma Majaji wastaafu linafanyika kwa mujibu wa Waraka Na. 1 wa Mwaka 2006 wa Jaji Mkuu.