Mwangalizi wa kanisa la Presbyterian of East Africa kwa Tanzania ,Mchungaji Franklin Msamila akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
Katibu mkuu wa kanisa hilo kwa Tanzania,Mchungaji Ibrahim Nnko akizungumzia kuhusiana na mkutano huo jijini Arusha.
Wachungaji hao wakifuatilia mkutano huo unaoendelea jijini Arusha .
………………………………
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.Zaidi ya wachungaji 500 kutoka kanisa la Presbyterian of East Africa kutoka nchi za Kenya ,Tanzania na Uganda wamekutana jijiji Arusha katika mkutano wa faragha wenye lengo la kujadili maswala mbalimbali pamoja na changamoto zinazowakabili.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa katika mkutano huo,Mwangalizi wa kanisa hilo upande wa Tanzania,Mchungaji Franklin Msamila amesema kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kuweza kujadili maswala mbalimbali yahusuyo huduma ya kanisani hilo yakiwemo ya kimwili na hata kiroho.
Amesema kuwa,wamekuwa wakikutana kila mwaka kwa ajili ya kujadili maswala mbalimbali ikiwemo changamoto wanazokabiliana nazo katika huduma hiyo na kuweza kuja na ufumbuzi sambamba na kujadili maswala mbalimbali yanayoendelea nchini na namna ya kuyapatia ufumbuzi.
Ameongeza kuwa,kama watumishi wa Mungu ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha wanatafuta muafaka wa maswala mbalimbali yanayoendelea kutokea sehemu mbalimbali hapa nchini yakiwemo ndoa za jinsia moja badala ya kukaa na kuongea tu .
“Unajua hili swala la ndoa za jinsia moja linaloendelea hapa kwetu sio wakati wa kuzungumza kila saa kuhusu jambo hilo bali tunatakiwa tutumie muda mwingi kumwomba Mungu atutoe katika janga hilo na kutafuta muafaka badala ya kuzungumzia jambo hilo kila wakati.”amesema .
Naye Katibu Mkuu wa kanisa hilo kwa Tanzania,Mchungaji Isaac Nnko amesema kuwa,kanisa hilo liko kwenye mikoa mitano Tanzania likiwa na jumla ya makanisa 25 ambapo alilitaka kanisa kutumika katika nafasi zao ipasavyo katika kumtumikia Mungu pamoja na kuhubiria watu kuacha matendo maovu yasiyompendeza Mungu.
Mchungaji Nnko amesema kuwa, hivi sasa maadili katika jamii yameharibika kwa kiwango kikubwa jambo ambalo linapelekea nchi kuelekea pabaya kutokana na kuongezeka kwa matukio mengi na ya kutisha ambayo yanamchukiza Mungu.
“Tunaomba sana wachungaji wajitahidi kuhubiri watu waache matendo maovu na sio kwa jijini tu waende na vijijini pia kwani wana nafasi kubwa ya kuhakikisha jamii inabadilika na kumrudia Mungu na kuacha maovu mbalimbali. “amesema Mchungaji Nnko.
Mwisho.