Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ametaja Utawala wa Haki unaokidhi Misingi ya Sheria, Uadilifu na Uwajibikaji, kuwa ni suluhisho kubwa la Mitafaruku ya Kisiasa hapa Nchini.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo, huko Ofisini kwake Migombani, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja, katika Maongezi yake na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Bw. Michael Battle.
Amesema kuwa hiyo inaweza kufikiwa kwa kuzingatia uoni sahihi pamoja na azma njema ya kuleta mageuzi ya kweli maeneo ambayo ni muhimu zaidi katika ujenzi wa utawala wa haki, hapa Nchini.
Ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Mifumo ya Chaguzi, Mahakama zenye Uadilifu, Haki Jinai, sambamba na Dhamira ya Kweli ya Kujenga Utulivu wa Kisiasa.
“Utawala wa haki ndiyo kila kitu katika kujenga utulivu wa kisiasa na pindipo tukikubaliana hayo kila jambo linakuwa rahisi katika kuleta maridhiano”, amesema Mheshimiwa Othman akifafanua namna Zanzibar ilivyokutana na mawimbi ya kisiasa tangu zamani na namna hatua za mageuzi zilivyokuja katika kukabiliana nayo.
Mheshimiwa Othman ameongeza kwa kusema, “suala la utulivu wa kisiasa ni muhimu, linahitaji kuungwamkono kwa hali na mali, kupitia mafunzo, taaluma na ufadhili na ikibidi kumfikia na kumuelewesha kila mtu katika jamii yote”.
Akifafanua kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) inayotawala sasa hapa Visiwani, Mheshimiwa Othman amebainisha hali ya kusogea kidogo, licha ya kuwepo hali ya kuchelewa kidogo kwa utekelezaji wa baadhi ya mambo na mapendekezo yanayoendana na matarajio ya wananchi wengi katika kuona Nchi yenye amani ya kudumu na siyo utulivu wa msimu.
“Kuna kusogea kidogo ‘progress’, watu wanaishi baina ya hofu na matumaini kwa yale yaliyowasibu hapo kabla; kwamba ni takriban miaka miwili imepita tangu Serikali hii (ya Awamu ya Nane) kuja madarakani, ‘atleast zipo initiatives zinazoonyesha willingness (khiyari na ridhaa), hatujasita, hatukati tamaa, tunaendelea kushinikiza hayo ili kujenga uaminifu na utawala wa kisiasa hapa Nchini”, amefafanua Mheshimiwa Othman.
Amefahamisha miongoni mwa utayari huo na juhudi zinazolea matumaini kwa kiasi fulani kuwa ni pamoja na Vikosi-Kazi alivyounda Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, vikiwemo vile vinavyolenga kupata Maoni Mahsusi yanayohusu Hali ya Kisiasa katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Katika maelezo yake, Mheshimiwa Othman amegusa suala la kuhamasisha maendeleo ya Nchi na Taifa kwa ujumla akisema bado vikwazo thakili vikiwemo ubadhirifu wa kupindukia na matumizi mabaya ya ofisi, ambayo amesema dawa yake ni kukusudia kwa dhati kuleta mageuzi, kujenga taasisi imara za kutoa haki zikiwemo Mahakama, na kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji.
“Unapokuwa na Mfumo wa Mahakama usiojali haki na uliosalitika usitarajie kwamba hata huo uwekezaji wenyewe kwamba utawezekana”, ameeleza Mheshimiwa Othman.
Amehimiza umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba, kwa Tanzania na Upande wa Visiwani, akifahamisha kwamba mara nyingi mahitaji hayo yanachukuliwa kwa hisia za kisiasa, bali lazima ieleweke kwamba Zanzibar, haiwezi kukiuka mahitaji hayo, kutokana na ukweli kwamba uwezo wake, ukiwemo wa kiuchumi, umekuwa ukidhoofika ndani ya Muungano, siku hadi siku.
Alipoulizwa kuhusu hitajio la Daraja la Baharini kati ya Tanganyika na Zanzibar, Mheshimiwa Othman amesema, ” hilo kwa sasa si kipaumbele cha Wazanzibari, bali yapo mahitaji mengi muhimu ya msingi na ya haraka kwaajili ya uchumi wa Nchi yakiwemo Ujenzi wa Bandari, Miundombinu, Usafiri na Upatikanaji wa Nishati ya Uhakika.
Aidha, amepongeza fungamano la tangu asili kati ya Marekani na Zanzibar, Kijamii na Kidiplomasia, akisema mahusiano hayo yalianza kabla ya takriban Mataifa yote ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, au hata Afrika yote.
Kwa upande wake, Balozi Battle ameeleza nia ya kuja na Ujumbe wake kuonana na Viongozi Wakuu hapa Visiwani kuwa ni pamoja na kuendeleza Mahusiano kupitia Biashara, Uwekezaji pamoja na Kuelewa Maendeleo ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.
Amesema yeye na Serikali ya Nchi yake wanaguswa na Mahitaji ya Utulivu wa Kisiasa hapa Nchini sambamba na hitajio la Mabadiliko ya Katiba, kutokana na ukweli usiopingika kwamba Zanzibar imekuwa haifurukuti, katika kujiendesha kiuchumi kwamujibu wa Mfumo uliopo sasa.
Katika Ujumbe wake Balozi Battle ameambatana na Maafisa Waandamizi kutoka Ubalozi wa Marekani Nchini, Bi Kristin Mencer na Bw. Colin Dreizin.
Wakati huo huo Mheshimiwa Othman, kwa nyakati tofauti, amekutana na Wasimamizi wa Taasisi za Fedha, pamoja na Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama Nchini, katika Vikao vilivyohusu kuwaarifu juu ya Mpango Mpya wa ‘Zanzibar Green Legacy’ unaolenga Kuirithisha Nchi Mazingira ya Kijani Yaliyosalimika.
Viongozi na Watendaji mbali mbali wamejumuika katika Vikao hivyo, wakiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Harusi Said Suleiman; na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Omar Dadi Shajak.