NDANI ya miaka miwili ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania madarakani hali ya mtandano wa barabara unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) umezidi kuimarika na kazi kubwa imefanyika baada ya kuongezeka kwa bajeti.
TARURA Mkoa wa Kilimanjaro unahudumia kilomita 4,659.93 ambapo kilomita 36.40 ni barabara mpya na kati ya hizo Barabara za Lami Kilomita 202.99, Barabara za Changarawe Kilomita 1,198.45 na Barabara za Udongo Kilomita 3,258.49.
Pia kati ya kilomita 4,659.93 za barabara, kilomita 1,767.3 ni za mjumuisho, kilomita 2,250.13 ni barabara za mrisho na kilomita 642.50 ni barabara za Kijamii.
Akizungumzia hali ya barabara, Meneja wa TARURA Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Nicholas D. Francis anasema, hali ya barabara zinazohudumiwa na TARURA Mkoa wa Kilimanjaro sehemu kubwa ni nzuri na wastani. Ambapo, kilomita 1442.62 sawa na asilimia 30.96 zipo katika hali nzuri, kilomita 1690.29 ikiwa ni asilimia 36.27 zipo katika hali ya wastani na kilomita 1527.02 ikiwa ni asilimia 32.77 zina hali mbaya.
Mhandisi Francis anasema kuwa kabla ya ongezeko la bajeti TARURA Kilimanjaro ilitengewa bajeti ya Sh bilioni 8.19 kwa mwaka 2020/21 kwa ajili ya matengenezo ya barabara.
Anasema kwa mwaka 2021/22, TARURA Mkoa wa Kilimajaro ilipata ongezeko la Sh bilioni 13.5 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo Sh bilioni 9.0 ni fedha za Tozo ya Mafuta (Sh. 100 kwa kila lita ya Mafuta ya Dizeli na Petroli) na Sh bilioni 4.5 ni fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali kwa ajili ya Miundombinu ya Barabara (kupitia Majimbo)
Akizunguzia bajeti na kazi zilizofanyikwa ndani ya miaka mwili ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia madarakani kwa kuanza na mwaka 2021/22, Mhandisi Francis anasema kuwa Sh bilioni 18.5 zilitengwa kwa ajili ya bajeti ya miradi maendeleo.
“Aidha, Serikali imekuwa ikituwezesha fedha za miradi ya dharura pale penye uhitaji ili kuweza kufanya barabara ziweze kupitika endapo inatokea uharibifu ambao haukuwekwa katika bajeti.”
Mhandisi Francis anasema TARURA Mkoa wa Kilimanjaro pia ulitengewa na kupokelewa Sh bilioni 8.222 kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum, sehemu korofi, matengenezo ya kawaida na ujenzi wa vivuko.
“Matengenezo maalum ni kilomita 57.70 kwa shilingi bilioni 1.182, sehemu korofi kilomita 249.73 kwa shilingi bilioni 3.381, matengenezo ya kawaida kilomita 1,039.59 kwa shilingi bilioni 2.039 na matengenezo ya vivuko na madaraja kwa shilingi milioni 784.76.”
Anasema pia TARURA Mkoa wa Kilimajaro ulitengewa Sh milioni 400.0 kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 0.80 ya barabara ya CD Msuya iliopo Wilaya ya Mwanga kwa kiwango cha lami.
Pia kupitia fedha za Tozo za Mafuta Sh bilioni 9.0 zilitengwa zimetengwa na hadi kufikia Juni, 2022 Sh bilioni 8.341 zilipokelewa hivyo kuwa na upungufu wa Sh milioni 659.216.
“Kupitia fedha hizi tumejenga barabara kwa kiwango cha lami kilomita 2.65 kwa shilingi bilioni 1.103, ujenzi kwa tabaka la mawe kilomita 6 kwa shilingi milioni 798.38 na ujenzi kwa kiwango cha changarawe kilomita 153.90 kwa shilingi bilioni 5.752.”
Mhandisi Francis anasema kwa fedha za jimbo Sh bilioni 4.5 zilitengwa na kutolewa na kujenga barabara kwa kiwango cha lami kilomita 1.73 kwa Sh bilioni 1.002, kilomita 6.8 kwa kiwango cha zege kwa shilingi milioni 350 na kwa kiwango cha changarawe km 73.97 kwa shilingi bilioni 2.71.
Kwa upande wa bajeti ya miradi maalum Mhandisi Francis anasema Sh milioni 629.59 zilitengwa kwa ajili ya kujenga kilomita 0.80 za barabara ya lami katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
Anasema kuwa kwa miradi ya dharura zilitengwa Sh bilioni 1.138 kwa ajili ya kujenga madaraja matatu katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai kwa gharama ya Sh milioni 540, barabara ya Mpirani Dispensary-Dindimo na Hedaru-Vunta-Myamba katika Halmashauri ya Wilaya ya Same kwa gharama ya Sh milioni 514 na ujenzi wa boksi kalvati moja kwa Sh milioni 133.2.
Akizungumzia kazi zilizofanyika kwa bajeti ya mwaka 2022/23, Mhandisi Francis anasema Sh bilioni 7.911 zilitengwa kwa ajili ya matengenezo ya kilomita 1,175.51 za barabara na vivuko 49 na mpaka sasa Sh bilioni 3.446 zimepokelewa.
“Hadi kufikia Februari mwaka huu, tumeshatengeneza mtandao wa barabara wenye kilomita 347.40 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.301 na ujenzi wa vivuko na matengenezo ya madaraja utakaotumika shilingi milioni 182.3 naWakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa miradi hii.”
Anasema kwa miradi inayotekelezwa na fedha za tozo, Sh bilioni 19.65 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilomita 10.77 na kwa kiwango cha changarawe kilomito 187.94 na hadi Februari, 2023 Sh bilioni 5.570 zilipokelewa.
Anasema hadi Februari, 2023, ujenzi wa km 1.8 kwa kiwango cha lami, km 29.58 kwa kiwango cha changarawe unaendelea na tayari Sh milioni 863.76 zimetumika.
Mhandisi Francis anasema kupitia fedha za majimbo Sh bilioni 4.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara kiwango cha lami kilomita 2.07 na changarawe kilomita 80.79 na tayari Sh milioni 795.667 zilipokelewa.
“Mpaka sasa umefanyika ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilomita 0.1 na ujenzi kwa kiwango cha changarawe kilomita 24.97 na shilingi bilioni 1.008 zimetumika.”
Kuhusu miradi ya maalum, Mhandisi Francis anasema zilitengwa Sh bilioni 5.0 kwa ajili ya ujenzi wa boksi kalvati 16 katika barabara ya CD Msuya (km. 13.8) iliyopo Wilaya ya Mwanga na mradi upo katika hatua za awali za utekelezaji.
Anasema kwa miradi ya dharura Sh bilioni 1.132 zimetengwa na kupokelewa kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Mpirani Dispensary-Dindimo Primary (4.3km) na Hedaru-Vunta-Myamba (0.83km) zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Same na miradi hiyo ipo katika hatua manunuzi.
Anasema baada ya ongezeko la bajeti katika miaka miwili ya Rais Samia, hali ya utekelezaji wa miradi ya barabara imeimarika kwa kiasi kikubwa ambapo barabara za lami na zege zimeongezeka kwa kilometa 20.57 na kiwango cha changarawe kiasi cha kilometa 138.17, na kupunguza urefu wa km 116.56 za barabara za udongo.
Akizungumzia mafanikio ya TARURA Mkoa wa Kilimanjaro kwenye miundombinu ya barabara hadi Februari mwaka huu, Mhandisi Francis anasema ni kuongezeka kwa mtandao wa barabara zenye hali nzuri na wastani kwa asilimia 5.52 hadi asilimia 63.52 ukilinganisha na asilimia 58 ya mwaka 2021.
Anasema pia bajeti ya TARURA Mkoa wa Kilimanjaro imeongezeka kutoka Sh bilioni 9.294 kwa mwaka 2020/21 hadi Sh bilioni 26.027 kwa mwaka 2021/22 na Sh bilioni 33.188 kwa mwaka 2022/23.
“Ofisi ya TARURA Mkoa wa Kilimanjaro hatuna budi kupongeza juhudi zinazofanywa na Wakala na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini na mjini.”
Kuhusu mikakati iliyopangwa Mhandisi Francis anasema: “kama ilivyo kaulimbiu yetu ya ‘TARURA tunakufungulia barabara kufika kusikofika’, ndivyo tunavyohakikisha thamani ya fedha iliyotengwa inaonekana ili kufungua barabara kufika maeneo yenye huduma za kijamii na fursa za kiuchumi.”
Anasema ili kuendelea kuboresha barabara kuwezesha kupitika katika kipindi chote cha mwaka, TARURA Mkoa wa Kilimanjaro umeweka kipaumbele cha kuondoa vikwazo katika barabara ambazo zilikuwa hazipitiki.
“Tumepanga kujenga madaraja kwa kutumia rasilimali za mawe kwa bei nafuu kama tulivyofanya katika Wilaya za Siha, Hai, Mwanga na Same na kufanya barabara zipitike kipindi chote, utaratibu huu tunaendelea nao katika kufikia malengo ya kufungua barabara zetu zote.”
Anasema pia TARURA Mkoa wa Kilimanjaro utajenga mifereji ya maji na vivuko ili kuzifanya barabara zidumu kwa muda mrefu kwa kutenga fedha kila mwaka kwa kazi hiyo.
Mhandisi Francis anasema pia wamepanga kutafuta maeneo kwa ajili ya kuchimba changarawe ili kupunguza ghara na fedha nyingi itumike kwa ajili ya kuboresha na kupandisha hadi barabara za udongo kuwa za changarawe.
Anasema pia awamepanga kutenga fedha kwa ajili ya kuweka taa za barabarani katika kuimarisha usalama kwa watumiaji wa barabara.
“TARURA Mkoa wa Kilimanjaro tunapenda kutoa Shukrani zetu za dhati kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanikisha kuboresha mtandao wa barabara zetu na kwa sasa barabara nyingi zilizokuwa zimeshindikana kutengenezwa kutokana na fedha kidogo zilizokuwa zikitengwa tumeweza kuziboresha na kufupisha muda wa safari kwa watumiaji wa barabara.”