Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akiongea na wajumbe (hawapo pichani) wa kamati ya maandalizi ya mkutano wa Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Kanda ya Nne (AUSC) Mei 02, 2023 jijini Arusha.
Na Eleuteri Mangi, WUSM, Arusha
Maandalizi ya Mkutano ngazi ya Mawaziri wa Michezo wa Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Kanda ya Nne (AUSC) utakaofanyika Mei 04, 2023 jijini Arusha yamekamilika na umetanguliwa na mkutano wa wataalamu wa sekta ya michezo miongoni mwa nchi zinazounda kanda hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema baadhi ya wajumbe wa Mkutano huo wamefika jijini Arusha tayari na wameridhishwa na maandalizi ya Mkutano.
Akiongea na wajumbe wa Kamati ya maandalizi Mei 02, 2023 Bw. Yakubu amesema Serikali imejipanga kufanyika kwa Mkutano huo ambao una Baraka zote za Viongozi Wakuu wa Nchi akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkutano huo unahusisha Nchi 14 za ukanda huo ambapo hadi Mei 02, Nchi nane tayari wajumbe wake ambao wanaunda Kamati ya wataalamu wamefika nchini ikiwemo Comoro, Djibout, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Shelisheli, Sudan Kusini, Uganda na wenyeji Tanzania kwa Mkutano huo wa siku mbili Mei 2-3, 2023 kabla ya Mkutano wa Mawaziri wenye dhamana na Michezo.