Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella (Katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Tawi jipya la Kwa Mrombo la Benki ya NMB katika hafla maalum ya uzinduzi wa Tawi hilo mkoani hapo. Tawi hilo linakuwa Tawi la 6 la Benki ya NMB kwa jiji la Arusha, na la 229 kwa nchi nzima. Wapili kushoto ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, wapili kulia ni Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania tawi la Arusha, Ibrahim Malogoi, kulia ni Naibu meya wa jiji la Arusha, Veronica Hosea na kushoto ni Mkuu wa Idara ya Mtandao wa matawi wa Benki ya NMB, Donatus Richard na Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Dismas Prosper.
…………………………….
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeipongeza Benki ya NMB kwa kuwa kinara miongoni mwa mabenki 44 nchini kwa ubunifu wa kuchangia ukuaji wa sekta ya fedha kwa kutanua mtandao wa matawi, hivyo kuongeza idadi ya watanzania wanaotumia huduma za kibenki, na hivyo kukuza kiwango cha amana za wateja.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa BoT Kanda ya Arusha, Ibrahim Malogoi, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB Kwa Mrombo jijini Arusha, ambalo linakuwa tawi la 229 kwa Benki hiyo nchini, hafla iliyohudhuriwa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi.
Uzinduzi wa Tawi la Kwa Mrombo linalokuwa la sita la Benki ya NMB jijini Arusha, huku likiwa ni la 12 kwa mkoa huo na la 43 Kanda ya Kaskazini, umefanyika leo, sambamba na makabidhiano ya msaada wa madawati 100 kupitia Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), kwa ajili ya Shule ya Msingi Msasani iliyopo jirani na tawi hilo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Malogoi alisema sekta ya fedha inakua kwa kasi kubwa nchini na kwamba wao kama ndio wasimamizi wakuu wa sekta hiyo Tanzania, wanafarijika kwa ongezeko la matawi ya benki nchini, huku akipongeza uamuzi wa NMB kufungua tawi Kwa Mrombo, eneo ambalo linakua kwa haraka na kuongezeka kwa uhitaji wa huduma za kibenki.
Kwa upande wake, RC Mongella alisema anaamini kuwa NMB Tawi la Kwa Mrombo ni kichocheo cha ukuaji kiuchumi kwa wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi wa Arusha, na kuwa uwingi wa matawi mkoani mwake, pamoja na uwekezaji mkubwa kidijitali uliofanywa na NMB, utaondoa foleni matawini zinazokwaza ustawi kiuchumi, hivyo kurahisisha mzunguko wa utafutaji na kuchochea fursa za maendeleo na kutoa wito kwa wana Arusha kutumia vema fursa za kustawi kiuchumi zinazoletwa na NMB.
Awali, Mponzi alimshukuru RC Mongella kwa kutenga muda wa kushiriki uzinduzi wa tawi hilo ambalo linaenda kuwa chachu ya maendeleo na mkombozi wa wateja wao, wakiwemo mawakala wa NMB waliotapakaa katika mji wa Arusha na mikoa mikoa jirani ya Kanda ya Kaskazini.
“Tunajivunia kukua kwa mtandao wetu wa matawi, sambamba na uwekezaji mkubwa kidijitali, ambao unampa fursa mteja kufungua akaunti kwa simu na hata kupata huduma, zikiwemo za Mikopo midogo isiyo na dhamana ya Mshiko Fasta,” alibainisha Mponzi mbele ya Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Matawi ya NMB, Donatus Richard na Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Dismas Prosper.
Lakini pia, aliushukuru Serikali kwa kuboresha mazingira ya taasisi za fedha kutoa huduma kwa ufanisi, na kwamba wanajivunia hilo wakati huu ambao benki yake inaadhimisha Miaka 25, sherehe zinazoenda sambamba na kampeni endelevu ya upandaji miti milioni moja kwa mwaka huu, iliyozinduliwa Machi mjini Dodoma na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango.