NDANI ya miaka miwili ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kumekuwa na ufanisi kwenye barabara zinazosimamiwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini Mkoa wa Mbeya hatua ambayo imerahisisha usafiri na usafirishaji.
Mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na uamuzi wa Serikali chini ya Rais Samia kuongeza fedha kwa ajili ya miundombinu ya barabara za wilaya hivyo kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa jumla.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Wilson Charles anasema ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia, bajeti ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara za wilaya imeongezeka kutoka Sh. bilioni 8.2 kwa mwaka 2021/22 hadi kufikia Sh. bilioni 17.96 kwa mwaka 2022/23, hivyo kuwezesha kuzifanyia matengenezo barabara zenye jumla ya urefu wa km 466.43.
TARURA Mkoa wa Mbeya una hudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya kilomita 4,512.24, madaraja 371, kalavati 2,609, boksi Kalavati 353 na madrifti 25.
Anasema hali ya barabara imezidi kuimarika baada ya kuongezwa kwa bajeti kwani barabara zenye hali nzuri zimeongezeka kutoka kilomita 417.57 hadi kufikia kilomita 883.16 ikiwa ni ongezeko la kilomita 465.41 sawa na asilimia 111.5.
Mhandisi Charles anasema barabara zenye hali ya wastani zimeongezeka kutoka kilomita 1,315.85 hadi kufikia kilomita 1,333.32 ikiwa ni ongezeko la kilomita 17.47 sawa na asilimia 1.3 wakati barabara zenye hali mbaya zimepungua kutoka kilomita 2,778.65 hadi kilomita 2,295.76 zikiwa zimepungua kilomita 482.89 sawa na asilimia 17.4.
“Kabla ya bajeti kuongezeka utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara ulikuwa katika ufanisi mdogo kwa kuwa barabara nyingi na za muhimu hazikufanyiwa matengenezo kwa sababu ya uhaba wa fedha.”
Anaongeza: “lakini baada ya kuongezeka bajeti, ufanisi umeongezeka kwa kuwa na mtandao mkubwa wa barabara unafanyiwa matengenezo na kurahisisha usafiri na usafirishaji, hivyo kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa jumla.”
Anasema kuongezeka kwa bajeti pia kumeongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi huku miradi mingi ikitekelezwa na kwa kiwango kizuri kwa kuwa kuna fedha ya kutekelezaji.
Mhandisi Charles anasema katika miaka miwili ya awamu ya Sita, pia kumekuwa na mafanikio ya ubora katika aina za barabara kwa kupandisha kiwango cha ubora.
Anasema TARURA Mkoa wa Mbeya umefanikiwa kujenga barabara za lami km 32.05 hadi kufikia kilomita 130.63 kutoka kilomita 98.58 sawa na asilimia 32.5.
Kwa upande wa barabara za changarawe zimejengwa kilomita 201.38 hadi kufikia kilomita 1,531.66 kutoka kilomita 1,330.28 sawa na asilimia 15 wakati barabara za udongo zimepungua kutoka kilomita 3,085,38 hadi kufikia kilomita 2,849.95 zikiwa zimepungua kilomita 233.43 sawa na asilimia 7.6.
Kufuatia nyongeza ya kiasi hicho cha fedha Mhandisi Charles anasema pia mafanikio yamepatikana katika matengenezo ya barabara, ambapo barabara za lami 2.55, changarawe 233.82, daraja kubwa moja, makaravati makubwa 12 makalavati ya kawaida 243 na madrifti 3 mwaka 2021/22 na mwaka 2022/23 barabara za lami 29.50 changarawe 214.10, mdaraja makubwa 4, makaravati makubwa 7, makavati ya kawaida 212 na madrifti 3.
Aidha, Mhandisi Charles anasema TARURA Mkoa wa Mbeya imeweka mikakati na kujiandaa kusimamia kwa weledi mkubwa utekelezaji wa miradi ya matengenezo na ujenzi wa barabara.
Anasema miongoni mwa maeneo muhimu ya kusimamia na kutekeleza kwa ufanisi mkubwa ni kuhakikisha kuwa barabara zote zenye hali nzuri zinafanyiwa matenegenezo na kuendelea na hali hiyo nzuri.
Mhandisi Charles anasema pia kuhakikisha kuwa maeneo yote muhimu hasa ya kutolea huduma za kijamii yanafikika kwa kuondoa vikwazo hasa kwa kujenga vivuko.
Pia kuhakikisha kuwa kiasi kinachotengwa kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya barabara kinatumika kama ilivyokusudiwa na kuleta manufaa kwa wananchi.
Mhandisi Charles anasema:” TARURA Mkoa wa Mbeya inatoa shukrani kubwa kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Tanzania kwa kuongeza bajeti ya matengenezo ya barabara za mkoa huu kwa miaka miwili mfululizo.”
“TARURA Mkoa wa Mbeya inamshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada na ahadi zake za kuongeza bajeti ili kuhakikisha kuwa barabara zinafanyiwa matenegenezo ili kuwanufaisha wananchi.”
Mhandisi Charles alitumia fursa hiyo kutoa ahadi ya TARURA Mkoa wa Mbeya ya kusimamia kwa weledi mkubwa matumizi ya fedha hizo ili kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mbeya inahudumia halmashauri saba ambazo ni Busokelo, Chunya, Kyela, Mbarali, Mbeya CC, Mbeya DC na Rungwe.