Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akizungumza na wataalam Kutoka Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Kanda ya Nne (AUSC) Katika mkutano unaofanyika jijini Arusha
…………………………..
Na Brown Jonas, WUSM Arusha
Tanzania ipo tayari na imeomba ridhaa ya kuwa Makao Makuu ya Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Kanda ya Nne (AUSC) kwa wajumbe wa mkutano wa wataalamu wa michezo kutoka katika kanda hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema hayo jijini Arusha wakati akifungua kikao cha wataalamu hao Mei 02, 2023 na kusisitiza kuwa Serikali ya Tanzania ina nia na kila sababu ya kuwa kmakao makuu ya kanda hiyo.
Mkutano huo wa wataalamu hao ni maandalizi ya kuelekea Mkutano wa Baraza hilo ngazi ya Mawaziri wenye dhamana na michezo atika kikao cha wataalamu wa michezo wa kanda hiyo kilichofanyika Jijini Arusha.
Katibu Mkuu Yakubu amesema ikiwa Tanzania itapewa ridhaa hiyo inauwezo wa kuhudumia sekratarieti hiyo iwapo wajumbe wa mkutano wataridhia kuichagua kuwa makao Mkauu.
“Kutokana na mipango thabiti iliyopo ndani ya Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluh Hassan ya kuendeleza diplomasia kupitia michezo, tunaomba kuwa makao makuu ya Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika ili kutekeleza azma hiyo ya Serikali amesema Yakubu.
Aidha, Bw. Yakubu ameeleza nia ya dhati ya Tanzania kuanzisha mashindano ya kanda hiyo pamoja na kuanzisha tuzo maalumu za michezo ndani ya kanda iwapo itachaguliwa kwa lengo la kusaidia kuinua michezo katika kanda hiyo.
Mkutano huo unafanyika kwa siku tatu kuanzia Mei 2 hadi 4, 2023 ambapo unatanguliwa na mkutano huo wa wataalamu na ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi Mei 04, 2023 jijini Arusha.