Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) Mhandisi Bernard Kavishe akizungumza na waandishi wa habari kuelekea kwenye mkutano wa mafundi sanifu utakao fanyika Jijini Mwanza Mei 4-5 mwaka huu.
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) Mhandisi Bernard Kavishe akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuelekea kwenye mkutano wa Mafundi sanifu utakao fanyika kwa siku mbili Jijini Mwanza
…….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Msajili wa Bodi ya Wahandisi Mhandisi Bernard Kavishe, amewasisitiza Wahandisi kuhuisha leseni zao ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi.
Ameyasema hayo leo Jumanne Mei 2,2024 wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelekea kwenye Mkutano wa Mafundi Sanifu utakao fanyika Jijini Mwanza Mei 4-5 mwaka huu.
Kavishe ameeleza kuwa baada ya tarehe 30 mwezi huu Bodi hiyo itatangaza majina ya Wahandisi waliohuisha leseni zao pamoja na Makampuni yao ili waweze kutambulika kwa wananchi na taasisi mbalimbali zitakazo hitaji kufanya nao kazi hapa nchini.
Amesema mada kubwa katika Mkutano huo ni mchango wa mafundi sanifu katika kutekeleza mpango wa kitaifa wa miaka mitano ya maendeleo ambapo mgeni rasmi anatarijiwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya ujenzi na Uchukuzi Balozi Mhandisi Aisha Amour.
” Taifa letu lina dira ya miaka mitano mitano na bajeti za kila mwaka hivyo ni lazima Kila fundi sanifu ajipambanue katika kufikia malengo na kuyavuka”, amesema Kavishe
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya siku ya Mafundi sanifu Mhandisi Benedict Mukama, amesema maandalizi ya Mkutano huo yamekamilika vizuri na zaidi ya Wahandisi 500 kutoka kanda ya ziwa watahudhuria.