NA MWANDISHI WETU
CHUO cha Furahika Education College kilichopo Buguruni Malapa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kimeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo kwa kutoa mafunzo ya ufundi bure kwa mabinti na vijana waliokatiza masomo yao kutokana na sababu mbalimbali nchini ili waweze kujikomboa kiuchumi.
Mkuu wa chuo hicho, David Msuya amesema, tayari wafadhili kupitia Serikali akiwemo Dokta Hellen kutoka nchini Ujerumani ametoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya mafunzo ya vijana wa kike na wa kiume waliofeli darasa la saba, kidato cha nne na sita.
“Tayari wafadhili kupitia Serikali wameshalipa ada wanachotakiwa watu wote wanapaswa kuleta vijana ili wapate mafunzo,”amefafanua Msuya.
Pia amesema, Furahika Education College wamesajiliwa na VETA na wanachofanya ni kutoa mafunzo hayo ikiwemo ushonaji,ufundi umeme,utalii,ustawi wa jamii,mafunzo ya biashara,malezi ya watoto,usafi, udarizi, udereva, urembo, muziki, kompyuta na mengineyo.
Amesema, kila mwanafunzi baada ya kuhitimu anatunukiwa cheti kinachotambulika na Serikali na kuingia katika soko la ajira aidha kwa kuajiriwa na kujiajiri mwenyewe popote pale nchini.
Mbali na hayo, kuhusu usajili wa wanafunzi chuoni hapo, Msuya ameeleza, fomu za kujiunga zinapatikana chuoni, Buguruni Malapa au kuwasiliana kwa simu namba 0778074099. “Usajili upo wazi kuanzia leo Mei 1, 2023 hadi Mei 18, 2023 ndipo dirisha litafungwa,”amefafanua Msuya.