NA FARIDA MANGUBE MOROGORO
Chama cha Waajiri Tanzania (ATE ) Kimeshiriki Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi ) yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro ambapo mwaka huu yamebeba kaulimbiu inayosema “Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi, Wakati ni Sasa.
Mgeni Rasmi katika sherehe hizo alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeambatana na viongozi mbalimbali wakuu wa kitaifa akiwemo za Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassimu Majaliwa Majaliwa ( MB), Mawaziri na Manaibu Waziri, Majaji, Mabalozi, baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi nchini na Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi.
Katika Hotuba yake, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Mei Mosi Siku ya kufurahia mchango wa wafanyakazi katika kujenga uchumi wa Taifa hivyo Serikali itaendelea kuboresha sekta ya Ajira kwa sekta za Umma na Binafsi pamoja kutatua changamoto zilizopo ili kuongeza tija na kujenga uchumi imara kwa maendeleo.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Rais pia amewapongeza ATE na TUCTA kwa kuwa mstari wa mbele kuendeleza ujuzi kwa vijana kupitia mafunzo ya Ufundi Stadi jambo ambalo lina manufaa makubwa kwa taifa letu.
Katika hatua nyingine Mhe. Rais ametaka waajiri wote nchini kuwasilisha michango mbalimbali ya wafanyakazi wao katika mamlaka husika kwani ni matakwa ya kisheria ili kuepuka udumbufu unaoweza kujitokeza kwa kushindwa kufanya hivyo.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako (MB) amesema kuwa Ofisi yake itaendelea kuimarisha utatu kwa kuhakikisha wanafanya kazi kwa Pamoja na ATE, TUCTA, ILO ili kuongeza ufanisi na kuchochea ukuaji wa Uchumi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ATE Bi. Jayne Nyimbo ambaye aliyeambatana na Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran akitoa salamu za Waajiri pamoja na mambo mengine amebainisha kuwa licha na juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali katika kuboresha mazingira ya Kazi na ajira nchini bado Waajiri wameendelea kukumbana na changamoto mbalimbali zinazorudisha nyuma juhudi hizo kama vile mlundikano wa kodi, uwepo wa sheria za kazi zisizoendana na wakati wa sasa hivyo kuiomba serikali kuzifanyia kazi changamoto hizi kwa ustawi wa uchumi.