Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Kaspar Mmuya akimkabidhi Nahodha wa timu ya kamba wanawake ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Dkt. Hawa Senkoro kombe la mshindi wa kwanza mchezo huo ulifanyika Aprili 29, 2023 kwenye hafla ya kuhitimisha Mashindano ya Kombe la Mei Mosi 2023 yaliyofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Kaspar Mmuya (kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa klabu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Neema Chilipweli kombe la mshindi wa jumla wa michezo ya Kombe la Mei Mosi katika hafla ya kuhitimisha michezo hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Timu ya kamba wanaume ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) wakiwavuta kwa mivuto 2-0 timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (kushoto) kwenye mchezo wa fainali wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliochezwa Aprili 29, 2023 katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Timu ya kamba wanawake ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi) wakiwavuta kwa mivuto 2-0 timu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) (kushoto) katika mchezo wa fainali ya michuano ya Kombe la Mei Mosi uliochezwa Aprili 29, 2023 kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
05. Mchezaji wa timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwanaisha Ally (GA) akijiandaa kupokea mpira uliorushwa na Bahati Mahenga (wapili kushoto) wakati wa fainali ya mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliochezwa Aprili 29, 2023 kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. Katikati ni Sophia Komba (C) wa timu ya Ofisi ya Rais Ikulu, ambaye timu yake imeshinda kwa magoli 37-36.
Mchezaji wa timu ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Anord Tryphone akimruka Golikipa wa timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Green Jairos wakati wa mchezo wa fainali wa soka uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro Aprili 29, 2023. Mambo ya Ndani ya Nchi wameibuka mabingwa kwa kushinda bao 1-0.
……………………………
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Mashindano ya Kombe la Mei Mosi 2023 yamehitimishwa mkoani Morogoro kwa timu zilizofanya vizuri katika michuano hiyo kwa kukabidhiwa makombe, medali na vyeti kwa timu zote zilizoshiriki mashindano hayo yakiwa ni shamrashara za kuelekea maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani.
Akifunga mashindano hayo mkoani Morogoro Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Bw. Kaspar Mmuya amesema mashindano hayo yamewasaidia watumishi kujenga afya ya mwili na akili na kuongeza ari ya kufanya kazi na kutoa huduma stahiki kwa wananchi katika maeneo yao ya kazi.
Bw. Mmuya amewataka waajiri kuendelea kuwapa fursa wafanyakazi kushiriki michezo ya Mei Mosi kila mwaka ikiwemo Wizara, taasisi, mikoa, wakala wa serikali, halmashauri, Ofisi za Wakuu wa Mikoa pamoja na sekta binafsi kutenga muda na kuwapa watumishi fursa ya kushiriki mashindano hayo kila mwaka yanapofanyika maadhimisho hayo kitaifa.
Akimkaribisha mgeni Rasmi katika hafla hiyo, Makamu Mwenyekiti Kamati ya Mei Mosi Taifa Bi. Roselyne Masamu amesema michezo ya mwaka huu imeshirikisha wanamichezo kutoka katika Wizara, mashirika na taasisi mbalimbali za umma na sekta binafsi kutoka klabu 39 wakiwa jumla ya wachezaji 2330 ambao wameshiriki michezo mbalimbali.
Bi. Masamu ameongeza kuwa Kamati ya Mei Mosi Taifa inahamasisha Wizara, Idara na taasisi ambazo hazikushiriki mashindano hayo watenge bajeti ambayo itawezesha timu zao kushiriki mashindano hayo ikizingatiwa michezo huleta hamasa katika utendaji kazi.
Katika kuhitimisha mashindano hayo timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imefanya vizuri katika michezo yake na kuibuka mshindi wa kwanza wa jumla huku ushindi wa pili umekwenda kwa timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi).
Aidha, katika hafla hiyo zimeshuhudiwa fainali za mchezo wa mpira wa miguu, netiboli pamoja na mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume na wanawake. Kwa upande wa mpira wa miguu bingwa ni timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, mshindi wa pili ni timu ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na mshindi wa tatu ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Kwa upande wa mchezo wa netiboli bingwa ni Ofisi ya Rais Ikulu wakifuatiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi huku nafasi ya tatu ikienda kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Katika mchezo wa kamba wanaume bingwa ni timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi), mshindi wa pili ni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na mshindi wa tatu ni Ofisi ya Rais Ikulu wakati kwa upande wa wanawake bingwa ni timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi), mshindi wa pili ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na mshindi wa tatu ni Wizara ya Afya.