Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
April 29
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini,Silvestry Koka amejielekeza kupeleka nguvu ya kifedha katika sekta ya elimu kwenye kata zote kwa asilimia 80 ya raslimali fedha yake.
Amesema ,anatambua sekta ya elimu Kuwa ni mkombozi na urithi namba moja katika Taifa lolote hivyo ataendelea kushirikiana na wazazi,walimu na jamii kutatua changamoto za kielimu.
Akizindua shule ya Sekondari ya Koka ,iliyopo kata ya Sofu ,Kibaha Mjini, Mkoani Pwani ambayo imepewa jina lake kutokana na mchango wake mkubwa kuchangia miradi ya kata hiyo.
“Asilimia 80 ya fedha zangu ,wadau wangu na mfuko wa Jimbo ninazielekeza katika elimu,fedha zangu binafsi,mfuko wa Jimbo kati ya fedha zangu ninazipeleka katika elimu kwenye kata zote, pili sekta ya afya na tatu miundombinu “
“Amshamsha kwa ajili ya elimu ,afya , barabara inaendelea na nitaendelea kuchapa kazi ,na nachokiomba wananchi watuunge mkono .”alisema Koka.
Mbunge huyo aliwataka wanafunzi shuleni hapo kuachana na ushawishi na kuachana na utoro ili kuongeza taaluma zao na kufaulu.
Vilevile Koka alieleza kazi kubwa waliianza kwa kupata eneo la kujenga shule,kufyeka na kuanza msingi na anashukuru ameweza kuchangia hatua mbalimbali kwa kutoa zaidi ya milioni 1.3 hadi sasa.
“Tupuuzie wale wachache wanaokebehi mambo tunayofanya,tutambue ukikebehi juhudi na utendaji kazi wa diwani,mbunge, Halmashauri unakuwa unabeza juhudi za Serikali “alifafanua Koka.
Koka alishukuru kwa heshima aliyoipata kwa mchango wake kata ya Sofu,na kudai amepokea kwa mikono miwili na ataendelea kuisimamia ili iwe bora katika miundombinu na kuinua taaluma.
Kwa Upande wa taaluma katika maandalizi ya mtihani wa kidato Cha pili ,walimu na wanafunzi ametenga milioni 3 kwa ajili ya kipindi cha maandalizi ya mtihani mwezi agost-octoba wakati wa mtihani.
“Neno la shule za kayumba liishe,sasa tuanze kuyumba na shule hizo nyingine,tujipange kufanikisha malengo yetu ya kuinua ufaulu”alibainisha Koka.
Amesisitiza mpango wa kujenga majengo ya shule hiyo kwenda juu ,ikiwa ni mpango wa muda mrefu wa kuimarisha na upanuzi wa shule ili eneo litoshe.
“Nimeongea na Waziri mwenye dhamana na amekubali kinachotakiwa kufuata taratibu ili kuanza mchakato wa mpango huo wa muda mrefu.”
Koka ameahidi kutatua tatizo la umeme shuleni hapo huku akihakikisha anapeleka Tanki la maji ya Lita 15 ili kupunguza tatizo la maji na atapeleka photocopy machine mashine ya kudurufu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha ambae pia ni diwani wa Sofu,Mussa Ndomba alieleza jina la Koka ni zawadi kwa utekelezaji wa Maendeleo katika kata hiyo.
Alishukuru pia kwa madawati 40 ya milioni 3.5 aliyochangia na kutoa milioni 3 kwa ajili ya umaliziaji kwenye madarasa.
Nae ofisa elimu sekondari Kibaha Mjini Rosemary Msasi, alieleza Halmashauri itahakikisha inatatua changamoto ziilizo ndani ya mipango ya halmashauri na kuna milioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa maabara.
Awali Mwalimu Mkuu shule ya Sekondari Koka ,Magreth William alisema kabla ya shule hiyo wanafunzi walitembea kimometa 4-5 kufuata elimu Nyumbu, kata ya Pichandege na Miembesaba ambako ni mbali.
Alieleza hadi sasa kuna wanafunzi 179 ambapo kidato Cha kwanza ni 115 na kidato cha pili 64.
“Katika robo mhula kidato cha kwanza wamefaulisha asilimia 88 na kidato cha pili asilimia 72 na wale waliopata 0 kidato Cha pili tutahakikisha tunawapiga Msasa na kudhibiti utoro”alifafanua Magreth.
Shule hiyo ina changamoto ya ukosefu wa umeme,uzio,tanki la maji na vitabu vya ziada na kiada.