Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Mh. Jerry Slaa akizunguma mara baada ya kukamilisha ziara ya kamati hiyo wakati ilipofanya ziara yakukagua miradi ya Shirika la Numba la Taifa NHC ya Morocco Square, Samia Housing Scheme Tanganyika Parkers na Kawe 7/11 Leo Jumapili Aprili 30 , 2023 jijini Dar es salaam kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Hamad Abdallah na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugeni wa shirika hilo Eliud Sanga.
…………………………………….
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetakiwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mashirika ya Ujenzi wa Nyumba nchini ili yaweze kuleta tija na kufikia malengo tarajiwa.
Akizungumza leo tarehe 29/4/2023 jijini wakati Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) walipotembelea miradi ya Shirika la Nyumba Taifa (NHC), Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Jerry Silaa, amesema kuwa serikali inapaswa kuwa makini wakati wa kufanya maamuzi pamoja na kuwaamini wakurugenzi wa mashirika ya Nyumba ili waweze kutekeleza majukumu kwa ufanisi kwa mujibu wa sheria ambazo zimewekwa na bunge.
“Muingiliano wa majukumu unaleta shida katika utekelezaji, tumeona mradi wa Morocco square , inabidi tuseme ili watanzania tusipate hasara” amesema Mhe. Silaa.
Mhe. Silaa amesema kuwa mahitaji ya Nyumba ni makubwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ni mkombozi mkubwa wa kuwasaidia watanzania kwa kuwajengea nyumba ikiwa katika hali ya ubora na bei nafuu.
“Ni jambo rafiki kujengewa nyumba na NHC kwani muda wa kusimamia ujenzi wa nyumba yako unakuwa unautumia kwenda kutafuta kipato chako kwa ajili ya kuendesha maisha yako” amesema Mhe. Silaa.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Taifa (NHC) Bw. Hamad Abdallah, ameishukuru kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa kutenga muda wa kutembelea miradi ambapo wameonesha wanathamini majukumu yao ya kusimamia utekelezaji wa miradi.
Bw. Abdallah amesema wamekuwa wakipokea ushauri mzuri kutoka kwa kamati kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wa miradi ya nyumba ili iweze kuwa tija.
Amesema leo wamekuwa na majadiliano ya utendaji wa Shirika la NHC na kamati ambapo wamejadili miradi mitatu ikiwemo Morocco Square ambao ni mradi wa kipekee ndani ya Tanzania na Afrika Mashariki.
“Huweze kukuta mradi mkubwa una sehemu ya Hotel, Shopping Mall ya kisasa, sehemu za maofisi pamoja na makazi ya watu katika jengo moja, ni jengo la kipekee na lenye ubora wa hali ya juu” amesema Bw. Abdallah
Mkurugenzi huyo amesema kuwa ndani ya muda mfupi wataaza kutumia jengo hilo kwa kuanza kutengeneza miundombinu ya watu kuanza kufanya shughuli mbalimbali za biashara.
Ameeleza kuwa mradi umekamilika kwa asilimia 97, huku asilimia 3 zilizobaki kwa ajili ni vitu vidogo vidogo ambavyo vinaaendelea kukamilika.
Bw . Abdallah amesema pia kamati imetembelea mradi wa Samia Housing Scheme ambao una Nyumba za kisasa 560 na unatarajia kumalizika mwisho wa mwaka huu.
Amesema kuwa kwa sasa mradi upo katika hatua ya ujenzi wa gorofa ya kwanza, huku akieleza kuwa mkandarasi anajenga gorofa moja kwa siku 15.
“Mradi tayari umeanza kuuza nyumba kwa asilimia 80, hali hiyo inaonesha kuna uhitaji mkubwa wa makazi Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania” amesema
Amesema kuwa pia kuna mradi wa Seven Eleven (711) ambao una Nyuma za kisasa 422, maeneo ya kufanyia biashara maduka makubwa na madogo pamoja na viwanja vya michezo.
Ameeleza kuwa mradi huo wa Seven Eleven ulisimama ujenzi tangu mwaka 2017 lakini kwa sasa umepata ushirikiano mkubwa kutoka serikali ya awamu ya sita na Julai mwaka huu mkandarasi anatarajia kuendelea na ujenzi.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Hamad Abdallah akiongoana na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo kushoto Bw Eliud Sanga na Mkurugenzi wa Uhandisi na Ujenzi NHC katikati mara baada ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kukagua mradi wa Samia Housing Scheme Tanganyika Pakers Kawe.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma wakiendelea na ukaguzi wa mradi wa Samia Husing Scheme.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Mh. Jerry Slaa akizunguma na wafanyakazi mara baada ya kukamilisha ziara ya kamati hiyo wakati ilipofanya ziara ya kukagua mradi wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Samia Housing Scheme Tanganyika Parkers Kawe.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Mh. Jerry Slaa akitoa maagizo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Hamad Abdallah akiongoana na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo kushoto Bw Eliud Sanga mara baada ya kukamilisha ziara ya kamati hiyo wakati ilipofanya ziara ya kukagua mradi wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC wa Kawe 7/11 Leo Jumapili Aprili 30 , 2023 jijini Dar es salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Hamad Abdallah akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Mh. Jerry Slaa pamoja na wajumbe wa kamati hiyo wakati wakikagua mradi wa Morocco Square jijini Dar es Salaam ambao umefikia asilimia 93 ya utekeleaji wake.