Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha,Eva Raphael aliyeko kulia akimkabithi dawa na vifaa tiba hivyo, Meneja wa TMDA mkoa wa Arusha Proches Patrick .
Baadhi ya dawa na vifaa hivyo vilivyokamatwa vikiingia nchini kwa njia ya magendo.
Kaimu Meneja wa TMDA, kanda ya kaskazini ,Proches Patrick akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .
Meneja wa TRA mkoa wa Arusha,Eva Raphael akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na swala hilo
…….
Julieth Laizer, Arusha.
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya kaskazini kwa kushirikiana na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) wamekamata dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya shs 88 milioni vilivyokuwa vinaingizwa nchini kwa njia ya magendo.
Akizungumza jijini Arusha baada ya kukamatwa kwa dawa na vifaa tiba hizo ,Kaimu Meneja wa TMDA kanda ya kaskazini, Proches Patrick amesema kuwa,mamlaka hiyo kwa kushirikiana na TRA walifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kukamata dawa na vifaa tiba hivyo vilivyokuwa vinaingizwa nchini kwa njia ya magendo.
Amesema kuwa,baada ya kukamatwa kwa dawa hizo watazifanyia uchunguzi ili kuweza kubaini kama zina ubora unaotakiwa na taratibu zingine kuweza kufuatwa.
Amesema kuwa, mamlaka hiyo imeweka wakaguzi wake katika vituo vyote vya Forodha vilivyopo kanda ya kaskazini ili kufanya ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara kabla bidhaa hizo hazijaingizwa hapa nchini.
Aidha amesema kuwa,katika dawa na vifaa tiba hivyo ,dawa zinagharimu shs 86,000,000 na vifaa tiba shs 2,000,000 ambapo amesema biashara za magendo sasa hivi zinazidi kupungua siku hadi siku kutokana na timu za patrol zinazofanya kazi vizuri katika maeneo mbalimbali.
“Madawa haya na vifaa tiba vilikamatwa na TRA vikiingia nchini kwa njia za magendo bila kupata vibali vinavyotakiwa na kukamatwa kwake ni kutokana na kuwa serikali ipo makini sana katika kuhakikisha hakuna yoyote anayeingia kimagendo nchini angeweza kuvuka kwenye mipaka hiyo kwani kwa kufanya hivyo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi yetu.”amesema.
Aidha amesema kuwa, kwa mfanyabiashara yoyote anayetakiwa kuingiza dawa nchini ni lazima bidhaa yake isajiliwe na iwe salama kwa mtumiaji kinyume na hapo hatua kali za kisheria lazima zichukuliwe dhidi yao .
Aidha alitoa onyo kwa wale wote wanaoingiza au kutengeneza bidhaa za dawa na vifaa tiba bila kuzingatia matakwa ya sheria ya Dawa na Vifaa Tiba,Sura 219 kuwa waache mara moja na TMDA haitamwonea huruma yeyote atakayebainika kukiuka matakwa ya sheria hiyo na kwamba wote watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za mtu yeyote anayeuza,kuingiza au kutengeneza dawa,vifaa tiba au vitenganishi bila kuzingatia sheria ya Dawa na Vifaa Tiba sura 219 ili waweze kuzifanyia kazi kwa siri kubwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria .
Kwa upande wake Meneja wa TRA mkoa wa Arusha ,Eva Raphael amesema kuwa, wafanyabiashara wanavyopitisha bidhaa hizo kwa njia za magendo kuna tuzo za TRA wanazotakiwa kulipia na za taasisi zingine na hivyo kuikosesha serikali mapato yake.
Amesema kuwa, baada ya kukabithi bidhaa hizo kwa TMDA na kuzifanyia ukaguzi na kuangalia kama zinafaa kwa matumizi zitachukuliwa na serikali kwa ajili ya hatua zingine zinazofuata.
“Mimi nawaomba tu jamani wale wote wanaofanya biashara hizo za magendo kuacha mara moja kwani serikali ipo makini sana ni vizuri kila mmoja wetu afanye kazi yake kwa kufuata sheria na taratibu za nchi ili kuepukana na hasara anayoweza kupata kama hizi za kutaifishwa bidhaa zake zote.’amesema Meneja.