Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya mwenendo wa ugonjwa wa Marburg uliogundukika mkoani Kagera hivi karibuni.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi Dkt. Grace Maghembe akifafanua jambo Katika mkutano huo.
Mganga mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam akijibu maswali kadhaa ya waandishi wa habari Katika mkutano huo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimaimiliza Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu hayupo pichani.
Na. WAF – Dar es Salaam
Taarifa zinaonesha kuwa Kuanzia tarehe 21 Aprili 2023 hakuna mgonjwa yeyote mwenye virusi vya ugonjwa wa Marburg Mkoani Kagera
Hayo ameyasema leo Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu alipokuwa anaongea na waaandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
“Wagonjwa wawili waliokuwa wamesalia katika vituo maalum vya matibabu waliruhusiwa kutoka tarehe 20 na 21 Aprili 2023 baada ya kuthibitika kimaabara kuwa hawana tena virusi vya Marburg.” Amesema Ummy Mwalimu
Waziri Ummy amesema hatua za haraka zilizochukuliwa na Serikali zilipelekea kuhakikisha ugonjwa huu wa Marburg hausambai nje ya familia zilizoathirika na kwa watumishi wa afya waliowahudumia wagonjwa kabla ya kuthibitika uwepo wa ugonjwa huo.
Sambamba na hilo, Waziri Ummy amesema kuwa tangu uwepo wa ugonjwa huo ulipotangazwa jumla ya watu waliopata maambukizi ni Tisa kati ya hao Watatu wamepona na wagonjwa Sita walipoteza maisha.
“Miongoni mwa waliopona ni pamoja na daktari aliyewahudumia wagonjwa wa mwanzo kabla ya kuthibitika, miongoni mwa watu waliopoteza maisha ni pamoja na mtumishi mmoja wa afya na mtoto mwenye umri wa miezi Tisa.” amesema Waziri Ummy
Katika jitihada za kuutokomeza ugonjwa huo Waziri Ummy amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea na ufuatiliaji wa magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Marbug.
“Endapo hakutatokea mgonjwa mpya mwenye virusi vya Marburg baada ya siku 42 yaani hadi ifikapo tarehe 31 Mei 2023 ndipo tutatangaza rasmi kumalizika kwa ugonjwa huu.” amesema Waziri Ummy
Hata hivyo, Waziri Ummy amewasisitiza watumishi wa afya juu ya kuzingatia Kanuni na miongozo ya Kuzuia na kudhibiti maambukizi kutoka kwa wagonjwa (IPC) wakati wote wa kuhudumia wagonjwa.
“Kwa unyenyekevu mkubwa ninamshukuru Rais. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kukabiliana na ugonjwa huu, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa kutuongoza vyema katika mapambano haya pamoja na Wataalamu wa afya na Wadau mbalimbali.” amesema Waziri Ummy