Baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam, Tegeta wakiwa darasani wakati wa mafunzo ya kujengewa uwezo katika nyanja mbalimbali ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mkurugenzi wa Kitengo Cha TEHAMA Chuo Kikuu Mzumbe, pia ni Mratibu wa Kitengo cha Digitalization mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation [HEET] Project), Dkt. Mohamed Ghasia akizungumzia mafunzo ya Wahadhiri wa chuo hicho namna itakavyosaidia kuboresha utendaji kazi wa utekelezaji wa majukumu ya kufundisha wanafunzi wa elimu ya juu.
Mhadhiri Msaidizi wa Masomo ya Uhasibu na Fedha Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam, Tegeta Bi. Jesca Kihanga akizungumzia mafunzo ya kujengewa uwezo waliopewa kupitia mradi (Higher Education for Economic Transformation [HEET] Project).
Baadhi ya Wakufunzi wakiwafundisha Wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam mambo mbalimbali ikiwemo Stadi za ufundishaji na kujifunzia, elimu mseto pamoja teknolojia ya kisasa katika kujifunzia.
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam wamejengewa uwezo kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao jambo ambalo litasaidia kuzalisha wahitimu wenye sifa katika soko la ajira na wenye uwezo wa kujiajiri.
Mafunzo hayo ya kuwajengewa uwezo yamefanyika kwa muda wa siku tatu kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation [HEET] Project) ambapo wamefundishwa mambo mbalimbali ikiwemo stadi za ufundishaji na kujifunzia, elimu mseto, kutumia teknolojia ya kisasa pamoja namna ya kuweka maudhui katika mfumo wa kujifunza wa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Akizungumza leo tarehe 28/4/2023 jijini Dar es Salaam katika mafunzo ya kuwajengea uwezo Wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam, Tegeta, Mkurugenzi wa Kitengo Cha TEHAMA Chuo Kikuu cha Mzumbe ambaye pia ni Mratibu wa Kitengo cha Digitalization Mradi wa HEET, Dkt. Mohamed Ghasia, amesema kuwa mafunzo hayo yanakwenda kuwasaidia wahadhiri katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuwafundisha wanafunzi wakiwa nje ya eneo la chuo kupitia mfumo wa mtandao.
Dkt. Ghasia amesema kuwa ili kuleta ufanisi wanaendelea kuboresha mitaala ya elimu ya juu kwa ajili ya kuzalisha wanafunzi wenye uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu masomo yao.
“Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa HEET ambao umelenga kuvijengea uwezo vyuo vikuu vya elimu ya juu nchini kwa ajili ya kuongeza wigo wa udahili” amesema Dkt. Ghasia.
Amesema kuwa wamezamilia kukiwezesha Chuo Kikuu Mzumbe katika kutoa elimu nje ya mipaka kwa kutumia elimu ya masafa, elimu ya mseto pamoja na elimu katika jamii kupitia kozi fupi.
Dkt. Ghasia amebainisha katika Chuo Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam wametoa mafumzo wa wahadhiri 25 ambapo wanaamini itakuwa chachu ya mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amefafanua kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kimeanza kutoa elimu ya masafa tangu mwaka 2009 kwa kuweka mfumo ya TEHAMA ambapo kwa sasa wanaendelea kuboresha ili kuleta tija.
“Tunaendelea kuwajengea uwezo wahadhiri katika Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mradi huu ambao una mambo mengi muhimu katika mafunzo ya elimu ya teknolojia, digital instructional for learning” amesema Dkt. Dkt. Ghasia.
Mkufunzi wa Somo la Mbunifu wa Mafunzo, Chuo Kikuu Mzumbe, Bi Halima Mwinyimkuu, amesema kuwa wahadhiri wamefundishwa namna ya kuweka maudhui katika mfumo wa kujifunza wa Chuo Kikuu cha Mzumbe jambo ambalo ni rafiki katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Nimewafundisha namna ya kufanya ubunifu wa kuweka maudhui ya kozi katika mfumo wa learning na kuifanya kozi iwe inapatikana katika mwaka wa masomo” amesema Bi. Mwinyimkuu.
Mkufunzi wa Elimu ya Sayansi wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Mustapha Almasi, amesema kuwa wahadhiri wamefundishwa stadi za ufundishaji na kujifunzia, elimu mseto pamoja teknolojia ya kisasa katika kujifunzia.
Dkt. Almasi amesema kuwa katika eneo la stadi limewajengea uwezo wahadhiri jinsi gani ya kumfundisha mwanafunzi wa elimu ya juu kwa kutumia mbinu za kisasa ikiwemo maswali, kuwashirikisha na teknolojia.
“Katika elimu mseto na teknolojia ya kisasa wamejifunza kwa namna gani teknolojia inaweza kumsaidia mwalimu kufundisha vizuri masomo yake” amesema Dkt. Almasi.
Dkt. Almasi amesema kuwa wahadhiri wamepata mafunzo ya matumizi ya teknolojia ambazo zitamuwezesha kufundisha mwanafunzi akiwa sehemu yoyote.
Mhadhiri Msaidizi wa Masomo ya Uhasibu na Fedha Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam Bi. Jesca Kihanga, amesema kuwa wamejifunza vitu vingi ambavyo vinakwenda kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kuwafundishwa mwanafunzi muda wowote kupitia mfumo wa mtandao.
Mafunzo ya kuwajengea uwezo wahadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaa, Tegeta yamefanyika muda wa siku tatu ambapo leo tarehe 28/4/ 2023 yamemalizika chuoni hapo.