…………………………..
Na Muhidin Amri, Songea
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas,amesikitishwa na baadhi ya wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule ya msingi Mkuzo Manispaa ya Songea,kushindwa kuchangia chakula cha mchana kwa ajili ya watoto wao.
Mkuu wa mkoa,amesema hayo jana wakati akizungumza na wanafunzi,walimu na baadhi ya wazazi wakati wa ziara yake ya kuhamasisha zoezi la upandaji miti katika Manispaa ya Songea mkoani humo.
Amewataka wazazi na walezi kuwa na huruma na kuona umuhimu wa kuanza kuchangia chakula ili kuwawezesha watoto kuwa na usikivu darasani jambo litakalowasaidia kufanya vizuri katika masomo yao.
Alisema,ni jambo lisilovumilika hata kidogo kuona mkoa wa Ruvuma unaongoza kwa kuzalisha chakula,lakini baadhi ya wazazi wanashindwa kuchangia chakula na hivyo kuwapa wakati mgumu walimu kutafuta chakula kwa ajili ya watoto hao.
Amewataka kubadilika kifkra na kuona aibu kwa kuwa hilo ni jukumu lao na siyo la serikali,hivyo ni lazima wawajibike kwa kuwapatia watoto wao mahitaji muhimu ikiwemo chakula na mavazi.
Aidha,Mkuu wa mkoa amepiga marufuku tabia ya wakulima kuuza mazao hasa mahindi yakiwa bado shambani,badala yake kusubiri hadi soko la uhakika litakapofunguliwa.
Alisema,ana taarifa kwamba wafanyabiashara wameanza kupita mashambani na kuwashawishi wakulima kuwauzia mahindi kwa bei ya Sh.1,000 hadi 1,200 kwa kilo moja ambayo hailingani na gharama ya uzalishaji mashambani.
Amewaonya wafanyabiashara kuacha mara moja tabia hiyo kwani serikali imejipanga kuchukua hatua kali kwa mtu na mfanyabiashara atayekamatwa anawarubuni wakulima ili wauziwe mahindi yakiwa bado shambani.
“ndugu zangu niwaambie mwaka huu mahindi yatakuwa na bei nzuri sana kwani baadhi ya mikoa ikiwemo Lindi,Mtwara,Pwani na Tanga hali ya uzalishaji wa chakula siyo nzuri kutokana na upungufu wa mvua”alisema.
Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa,kutokana na changamoto hiyo mahitaji ya chakula katika maeneo hayo ni makubwa,na kuwasihi wakulima kuendelea kuvuta subira hadi soko la uhakika litakapofunguliwa.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Songea Wilman Ndile alisema,serikai ya wilaya imejipanga kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anayekwenda mashambani kushawishi wakulima ili auziwe mahindi na mazao mengine yakiwa bado shambani.