Serikali imepiga marufuku wananchi wanaovamia na kujenga eneo la hifadhi ya Serikali ilipojengwa Rada kata ya Kiseke wilayani Ilemela jijini Mwanza
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masala katika viwanja vya shule ya sekondari Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuhamasisha maendeleo ambapo amesema kuwa Serikali itasimamia sheria kwa wavamizi wa maeneo ya Umma na kwamba haitavumilia viongozi wasio waadirifu wanaouza maeneo hayo na kusababisha migogoro ya ardhi isiyo ya lazima kwa wananchi
‘”Kuna viongozi wa mitaa wanashiriki kuuza maeneo ya Umma, Hawa hatuta waacha sheria itafuata mkondo wake, Lakini wapo pia wananchi wenzetu wanaojenga pale mlima wa rada wakati tulishakataza ndani ya zile mita 60,”. Alisema Masala.
Aidha Mhe Masala mbali na kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Ilemela utatuzi wa kero ya Maji na kwamba Serikali imeshatoa fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kwaajili ya usambazi Maji kutoka Tanki kubwa la Buswelu
Kwa upande wake mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ambae pia ni Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Charles Samson Marwa amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Marburg na Kipindupindu kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha
Nae mwakilishi wa Afisa elimu manispaa ya Ilemela Mwl Recipitius magembe amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni mia sita kwaajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari eneo la PPF Kiseke na eneo limeshatengwa kwaajili ya ujenzi huo
Thadeus Francis ni mkazi wa mtaa wa Zenze kata ya Kiseke ambapo amelalamikia changamoto ya ubovu wa barabara na ukosefu wa maji ndani ya mtaa wake
Mkuu wa wilaya ya Ilemela ataendelea na ziara yake katika kata nyengine zilizosalia akiambatana na wataalam wa manispaa na taasisi nyengine za Serikali za ndani ya wilaya hiyo