WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amelitaka Jeshi la Polisi kuchunguza matukio yote yaliyotolewa taarifa kuhusu kuteswa, kuumizwa na kuuawa kwa baadhi ya Wananchi waliotuhumiwa kuingia ndani ya hifadhi na watakaobainika wachukuliwe hatua stahiki.
Ametoa agizo hilo leo Alhamisi (Aprili 27, 2023) Bungeni Jijini Dodoma wakati akitoa maelezo kuhusu changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika kusimamia masuala ya uhifadhi.
Amesema kuwa Operesheni zote katika maeneo ya hifadhi zifanyike baada ya wananchi wa maeneo husika kushirikishwa na kupewa taarifa za kutosha na sio kuvizia “Kufanya hivyo kutaiwezesha Serikali kuendelea kuimarisha uhifadhi endelevu kwa ajili ya ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wahifadhi wahakikishe wanazuia mapema wananchi kuanzisha shughuli za kilimo, ufugaji na makazi ndani ya hifadhi “mkifanya hivi tutaepuka uhitaji wa kuondoa shughuli ambazo zimeshaanzishwa kama vile kuvunja makazi, kufyeka mazao au kukamata mifugo”
Kadhalika, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii ifanye ufuatiliaji wa malalamiko ya wananchi kuhusu tabia ya baadhi ya wahifadhi kuswaga mifugo na kiingiza hifadhini kwa lengo la kuitafisha na kujipatia fedha. “ Chukueni hatua kali kwa watumishi watakaobainika kufanya vitendo hivyo”
Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Wananchi wenye malalamiko ya kunyang’anywa mali, mifugo au kujeruhiwa watoe taarifa ya matukio hayo kwa wakati katika vituo vya polisi na Mamlaka za Wilaya ili Serikali iweze kuchukua hatua. “Nitoe rai kwa wananchi wenzangu kuzingatia sheria hususan zinazosimamia masuala ya uhifadhi na kuheshimu mipaka”.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya Serikali katika kuimarisha shughuli za uhifadhi endelevu, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa watalii wameongezeka kutoka Milioni 1.07 mwaka 2012 hadi kufikia Milioni 1.45 mwaka 2022.
“Vilevile, katika kipindi hicho mapato yatokanayo na Watalii wa Kimataifa yameongezeka kutoka Dola za Marekani Milioni Elfu moja mia saba kumi na mbili (1,712) hadi Dola za Marekani Milioni Elfu mbili mia tano ishirini na saba (2,527)”