Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-Maamary Mwamba, (kulia), akisalimiana na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Norgaard Dissingspandet, walipokutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi za Hazina Ndogo Jijini Dar es Salaam, ambapo Denmark imeahidi kuendelea kuipa ushirikiano Tanzania kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza sekta ya afya, kusaidia AZAKI na usimamizi wa fedha.
Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Norgaard Dissingspandet, (kushoto), akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu El-Maamary Mwamba, (kulia), walipokutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi za Hazina Ndogo Jijini Dar es Salaam, ambapo Denmark imeahidi kuendelea kuipa ushirikiano Tanzania kwa kutoa fedha zaidi katika sekta ya afya.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu El-Maamary Mwamba (kulia) akizungumza na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Norgaard Dissingspandet walipokutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi za Hazina Ndogo Jijini Dar es Salaam, ambapo Denmark imeahidi kuendelea kuipa ushirikiano Tanzania kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuendeleza sekta ya afya.
Ujumbe wa Tanzania na Denmark wakiwa katika mazungumzo katika Ofisi za Hazina Ndogo Jijini Dar es Salaam, ambapo Denmark imeahidi kuendelea kuipa ushirikiano Tanzania kwa kutoa fedha zaidi katika sekta ya afya. Ushirikiano wa Tanzania na Denmark umetimiza zaidi ya miaka 60 na kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuanzisha ushirikiano na Serikali ya Denmark ikiwa ni baada ya mwaka mmoja tu tangu Bunge la nchi hiyo lipitishe sheria ya Ushirikiano wa Kimataifa ,mwaka 1962.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu El-Maamary Mwamba (katikati), Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Norgaard Dissingspandet, (kushoto), na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban (kulia), wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo yao katika Ofisi za Hazina Ndogo Jijini Dar es Salaam, ambapo Denmark imeahidi kuendelea kuipa ushirikiano Tanzania kwa kutoa fedha katika sekta ya afya na kuchangia Bajeti ya Serikali
…………………………………………………
Na Joseph Mahumi, WFM, Dar es Salaam
Denmark imeahidi kuendeleza ushirikiano zaidi na Tanzania katika jitihada zake za kuimarisha uchumi na maendeleo ya wananchi kwa kutoa fedha na misaada ya kiufundi katika sekta ya mbalimbali ikiwemo afya.
Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mhe. Mette Norgaard Dissingspandet alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-Maamary Mwamba, katika Ofisi Ndogo za Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam.
“Denmark imekuwa ikishirikiana na Tanzania kwa miaka mingi kwa kusaidia utekelezaji wa bajeti ya Serikali, kusaidia ujenzi wa mifumo ya udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali, kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi na masuala ya afya kupitia ubia wa sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kwenye Asasi zisizo za Kiserikali (AZAKI) ambapo ushirikiano huo umeleta matokeo chanya kwenye sekta hiyo” alisema Mhe. Mette
Mhe. Mette amepongeza juhudi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusimamia maendeleo na kukuza uchumi wa nchi na maendeleo ya watu kwajumla.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu El-Maamary Mwamba ameishukuru Denmark kwa ushirikiano na mchango wao mkubwa katika kuendeleza sekta ya afya na kuahidi kuwa Tanzania itaendelea pia kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma nzuri katika sekta ya afya na kutumia fursa za ushirikiano wa nchi hizo mbili kuwahudumia Watanzania.
Ushirikiano wa Tanzania na Denmark umetimiza zaidi ya miaka 60 na kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuanzisha ushirikiano na Serikali ya Denmark ikiwa ni baada ya mwaka mmoja tu tangu Bunge la nchi hiyo kupitisha sheria ya Ushirikiano wa Kimataifa mwaka 1962.