Na WMJJWM Iringa.
Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha mkoani Iringa kimeandaa Mdahalo wa wazi wenye lengo la kushirikiana na Jamii kupata ufumbuzi wa suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Akifungua Mdahalo huo wa wazi Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha Jamii inarudi katika Maadili ya kitanzania kwa kuishirikisha ili iweze kuchukua jukumu hilo kwani Malezi ma Makuzi ya Watoto yanaanzia katika familia na jamii.
Ameongeza kuwa mmomonyoko wa maadili ni changamoto kubwa inayosababisha kuwa na jamiiyenye ukatili na isiyowajibika katika maendeleo yake na ya Taifa kwa ujumla.
” Tunaona sasa hivi katika jamii Watoto wamekuwa hawashikiki wazazi wamekuwa wakipambana na kutafuta maisha zaidi kuliko kuwasaidia Watoto wao waishi katika maadili mema” alisema Mhe. Halima.
Akizungumza katika Mdahalo huo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza kuipeleka Ajenda ya Linda Maadili kwa wadau mbalimbali ikiwemo wasanii wanamichezo na jamii kwa ujumla ili liwe suala la kitaifa na Kila mtanzania awe na kuchangia katika kupambana na mmomonyoko wa maadili nchini.
Katika mdahalo huo mada iliyojadiliwa ni “mmomonyoko wa maadili nchini Tanzania” huku wananchi, wanafunzi wa shule ya sekondari ya Tagamenda, viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa, watumishi na wanachuo wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha walishiriki kwa kujidiliana.
Mdahalo huo umeainisha visababishi vya mmomonyoko wa maadili nchini na athari zake katika jamii, washiriki wa mdahalo huo walitoa maazimio ambayo yatatekelezwa ili kumaliza au kupunguza kasi ya mmomonyoko wa maadili nchini.