Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Aprili 25, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikikata utepe kuashiria uzinduzi wa Baraza la Taifa la Kupambana na Maambukizi ya Malaria baada ya kuhutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duaniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Aprili 25, 2023. Kulia ni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Leodgar Tenga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Baraza la Taifa la Kupambana na Maambukizi ya Malaria baada ya kuhutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duaniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Aprili 25, 2023. Kulia ni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Leodgar Tenga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi pamoja na wajumbe wa Baraza la Taifa la Kupambana na Maambukizi ya Malaria baada ya kuzindua Baraza hilo katika Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Aprili 25, 2023. Kulia kwake ni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Leodgar Tenga. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza, mratibu wa masoko wa kampuni ya kutengeneza dawa ya kuangamiza mbu iitwayo Tanzania Biotech Products Limited, Pilly Abbas (kulia) wakati alipotembelea banda la kampuni hiyo kabla ya kuhutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Aprili 25, 2023. Wa pili kulia ni Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, Mhandisi Raphael Rodriguez. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………….
Na John Bukuku- Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa amewashukuru wadau wote wa malaria nchini kwa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria ambao umepoteza Maisha ya watanzania, leo Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku hii muhimu ambayo huaadhimishwa Aprili 25 kila mwaka.
Amefurahishwa na kauli mbiu ya maadhimisho hayo ambayo inasema ‘ Wakati wa kutokomeza malaria ni sasa badilika, wekeza, tekeleza zero malaria inaanza na mimi, inaanza na wewe na inaanza na wote”
Mh. Waziri Mkuu ameyasema hayo leo katika maazimisho ya siku ya kutokomeza Malaria duniani yaliyofanyika kwenye uwanja wa Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam leo Aprili 25,2023.
Amesema Kauli Kauli mbiu hiyo imebeba ujumbe muhimu sana katika mapambano haya hasa kutambua mchango uliofanywa na Serikali na uwekezaji mkubwa uliopo kuelekea katika kutokomeza malaria ifikapo 2030 na msisitizo uliotolewa katika ilani ya CCM ibara ya 83 (M) na (O).
“Nina hakika azimio la zero malaria linaloanza na mimi, wewe na wote linawezekana kabisa kutokemeza malaria nchini, takwimu zinasema maambukizi yameendelea kupungua nchini kutoka asilimia 15.8 mwaka 2015 hadi 8.1 mpaka sasa,” Amesema Mh. Kassim Majaliwa.
Ameongeza kuwa bado inahitajika nguvu kubwa katika mapambano haya kwani kwa miongo kadhaa ugonjwa huu umeendelea kupunguza nguvu kazi ya Taifa na kuleta athari kubwa hasa kwenye sekta ya uchumi na jamii.
“Nimearifiwa hapa mikoa inayoongoza kwa maambukizi ni Tabora asilimia 23, Mtwara 20 Kagera 18 Shinyanga 16 na Mara asilimia 15, nitoe wito kwa mikoa hii ihakikishe inasimamia kikamilifu afua za malaria ili kufikia malengo ya kutokomeza malaria ifikapo 2030.
“Nina taarifa kuwa mikoa 9 imefanya vizuri katika mapambano ya malaria kwa kuwa na chini ya asilimia 1 kwenye maambukizi ambayo ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Singida, Dodoma, Songwe, Iringa, Dar es Salaam na Mwanza mikoa hii imefanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa unapunguza malaria nchini chini ya asilimia 1,” Amesema Mh. Majaliwa.
Ametanabaisha kuwa Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa unafuu kwa watanzania kupata huduma bure ikiwemo kipimo cha malaria (MRDT), dawa za Alu, Sindano ya malaria kali na dawa wanayotumia wajawazito (SP) huu ni mkakati wa kutokomeza malaria nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mawlimu akizunguma katika maadhimisho hayo amesema asilimi 96 ya dawa za malaria zina uwezo wa kutibu malaria, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya dawa za malaria ili kuwezesha mapambano dhidi ya malaria yanawezekana na Tanzania kuwa na zero malaria.
Mh. Ummy Mwalimu amesema kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameunda Baraza la Taifa la kupambana na malaria ambalo lina wajumbe 19 likiongozwa na Leodgar Tenga huku wajumbe wake wakiwa ni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na wajumbe wengine kutoka Wizara husika.
“Katika Kila watu 100 Tanzania watu 77 wana umri chini ya miaka 35 kwa hiyo asilimia 77 ya Watanzania ni vijana na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua ndugu Nasib Abdul maarufu kama Diamond kuwakilisha vijana katika mapambano haya,” Amesema Mh. Ummy Mwalimu.
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Wizara ya Afya inatushirikisha vya kutosha katika vita hii ya mapambano dhidi ya malaria na kuna kazi nzuri inafanya na Waziri Ummy Mwalimu na timu yake na sisi tunamuunga mkono kuhakikisha tunatokomeza malaria katika nchi yetu na inawezekana.
Kama Waziri ambaye mmenipa jeshi kubwa la Habari, mmenipa jeshi kubwa la mitandao ya kijamii na jeshi kubwa la Mawasiliano katika nchi hii nataka niwaelekeze wanahabari na vyombo vyote vya Habari katika nchi hii mnakuwa na mpango wa kuhakikisha Tanzania inakuwa na zero malaria.