Diwani wa Kata ya Kijitonyama, Dama Samora Lusangija.
…….
Jumla ya timu 20 zinatarajia kushiriki katika mashindano ya kuwania kombe la Diwani wa Kijitonyama (Diwani Cup) lilolopangwa kufanyika mwezi Juni mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Diwani wa Kata ya Kijitonyama, Dama Samora Lusangija alisema kuwa kwa sasa wapo katika maandalizi ya mashindano hayo ambapo lengo kuu ni kuinua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi katika kata hiyo.
Lusangija alisema kuwa timu hizo zitagawanyika katika makundi manne zenye timu tano kila moja huku viwanja vya Vinyago, Shule ya msingi Mapambano, Shule ya Msingi Kijitonyama Kisiwani na uwanja wa Bora vitatumika.
Alisema kuwa ili kuhamasisha wachezaji hapo chipukizi, kamati ya mashindano hayo imeruhusu wachezaji watatu wanaoshiriki ligi kuu ya Tanzania Bara kucheza.
Alifafanua kuwa wachezaji hao wanatakiwa kusajiliwa kabla ya mashindano na hawataruhusiwa kuchezea timu nyingine. Baada ya kupitishwa katika usajili wao
“Kila timu itatakiwa kusajili wachezaji 16 ambapo kati ya hao, wachezaji watatu wanatakiwa kuwa wa ligi kuu, timu inaweza kusajili au kuacha kusajili. Tunaomba makampuni mbalimbali kusaidia mashindano hayo,” alisema Lusangija.
Aliziomba timu ambazo zitashiriki kuanza mazoezi kuelekea katika mashindano hayo ambapo mbali ya zawadi kwa mshindi wa kwanza, pili na wa tatu, pia kutakuwa na zawadi za mfungaji bora na mchezaji bora wa mashindano.