Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza leo tarehe 24/4/2023 jijini Dar es Salaam wakati akizindua Kamati ya Ushauri wa Maendeleo ya Viwanda (IAC) kwa ajili ya utekeleza Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation [HEET] project) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kutekelezwa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Profesa William Mwegoha akizungumza leo tarehe 24/4/2023 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Maendeleo ya Viwanda (IAC) kwa ajili ya utekeleza Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation [HEET] project) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na kutekelezwa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Mratibu wa Mradi Elizabeth Mwakasungula akizungumza jambo kuhusu Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation [HEET] project) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Wajumbe wa Kamati ya Ushauri wa Maendeleo ya Viwanda (IAC) kwa ajili ya utekeleza Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation [HEET] project) wakiwa katika picha ya pamoja.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameitaka Kamati ya Ushauri wa Maendeleo ya Viwanda (IAC) kufanya tafiti kuhusu mitaala ya elimu ya juu nchini inayotumika jambo ambalo litasaidia kuzalisha rasilimali watu kulingana soko la ajira linavyotaka.
Imeeleza katika kutekeleza Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi yaani (Higher Education for Economic Transformation [HEET] project) ambao unaofadhiliwa na benki ya Dunia na kutekelezwa Chuo Kikuu Mzumbe ambapo leo kamati ya ushauri wa Maendeleo ya Viwanda (IAC) imezinduliwa rasmi kwa ajili ya kuangalia mambo mbalimbali ya utekelezaji wa mradi kwa ufanisi.
Akizungumza leo tarehe 24/4/2023 jijini Dar es Salaam wakati akizindua Kamati ya Ushauri wa Maendeleo ya Viwanda (IAC) Dkt. Kijaji, amesema kuwa kamati inapaswa kukaa chini na kuangalia ni wapi duniani inaelekea na kupanga mkakati kulingana na soko la ajira ili wazalisha wahitimu watakaofanya vizuri sokoni.
Dkt. Kijaji amesema kuwa kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa waajiri kuhusu waajiriwa wengi hawana sifa katika soko la ajira.
“Nimekaa vikao na wamikiki wa viwanda, sekta binafsi, taasisi mbalimbali malalamiko ni hayo hayo wasomi wetu hawana sifa, hivyo wanalazimika kuwafundisha tena nje ya nchi ili waweze kuwatumia katika kufanya kazi zao” amesema Dkt. Kijaji.
Amesema kuwa kamati inawajibu kwenda kuangalia ni kitu gani tumekosea na tupo wapi, kwani watu wengi wamekuwa wakiwashangaa baadhi ya wahitimu wakiwa katika soko la ajira.
Amesema wakati umefika wa kamati kufanya kazi kwa uweledi kwa kutoa ushauri katika Chuo Kikuu cha Mzumbe ili kuleta matokeo chanya kwa taifa.
”Tunapoingia katika soko la afrika tuwe washindani na sio washiriki kupitia rasilimali watu ambao tunawapeleka katika soko la ajira”
Amefafanua tunapaswa kuwandaa rasilimali watu kulingana na soko la ajira kwa sasa na baadaye jambo ambalo litasaidia kufikia malengo tarajiwa.
Ameeleza kuwa tupo katika mageuzi ya nne ya viwanda hivyo mitaala yetu inaendana na uhitaji wa sasa katika soko la ajira.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Profesa William Mwegoha, amesema kuwa wana jukumu la kuzalisha wataalamu katika fani wenye sifa mbalimbali ili kuleta tija kwa taifa.
Profesa Mwegoha amesema chuo hicho kimepewa dola za Marekani Milioni 21 ili kutekeleza mradi huo, asilimia 80 na fedha hizo ni kwaajili ya ujenzi wa miundombinu na asilimia 20 ni kwaajili ya kutekeleza mambo mengine ikiwemo kuendeleza wanataaluma.
Amesema kuwa Katika mradi huo wataanzisha mbinu bunifu za kufundishia ikiwa ni pamoja na kuboresha mitaala ya kufundishia na kujenga ushirikiano na Sekta ya viwanda pia kuwa na atamizi ya kuwanoa wataalamu mbalimbali watakaoenda kufanya kazi katika viwanda hapa nchini.
“Ili kutatua changamoto ya ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko na uchumi wa sasa kwa wahitimu wetu, sisi Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), tumedhamiria kujenga muunganiko imara katika ya elimu ya juu na viwanda” amesema Profesa Mwegoha.
Amesema kuwa kupitia mradi huu wanatarajia kajenga mashirikiano, ubia, na kuendesha shughuli za pamoja na viwanda ambazo zitawawezesha wanafunzi na wafanyakazi kupata ujuzi na uzoefu kupitia kushughulika na changamoto halisi zinazotokea katika viwanda na soko la ajira.
Mratibu wa Mradi Elizabeth Mwakasungula, amesema kuwa pia mradi umelenga kuwajenga uwezo wa wafanyakazi pamoja na uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mafunzo mbalimbali.
Amesema kuwa wanatarajia kutoa elimu kwa jamii kuhusu masula mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchini.
“Tayari tumeanza kutekeleza mradi huu kwa kuwashirikisha wataalamu mbalimbali pamoja na kuweka mazingira rafiki ili kuhakikisha malengo yanafanikiwa” amesema Mwakasungula.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Mzumbe, amesema kuwa wataenda kuyafanyia kazi maelekezo waliyopewa ikiwa ni pamoja na kujifunza kwa bidi ili kuendeleza taifa kwa vitendo.
Mradi huo unatekelezwa nchini kupitia Wizara ya Elimu sayansi na Teknlojia hapa nchini kwa upande wa Chuo kikuu Mzumbe, Kamati hiyo ya Ushauri wa Viwanda ni ni sehemu ya utekelezaji katika mradi huo ukiwa na malengo ya kujenga muunganiko mzuri na imara kati Chuo Kikuu Mzumbe na Sekta ya Viwanda katika kutoa ushauri na kushirikisha uzoefu juu ya maendeleo ya viwanda.