Na WMJJWM, Dar Es Salaam.
Viongozi wa Dini, Wahariri wa Habari na Wadau mbalimbali wamebainisha sababu zinazochangia mmomonyoko wa maadili nchini na kuiasa jamii kurudi kwenye Maadili yanayozingatia Mila na Desturi.
Hayo yameelezwa wakati wa kikao cha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima na Viongozi hao kwa lengo la kujadili changamoto ya Mmomonyoko wa Maadili katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 24 Aprili, 2023 jijini Dar Es Salaam.
Wadau hao wakijadili mada zilizowasilishwa kuhusu maadili, wamesema malezi ya sasa yana changamoto kutokana na utandawazi, ukuaji wa teknolojia na wazazi kushindwa kuwajibika.
Akizungumza kwa niaba ya Jukwaa la Wahariri, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Bakari Machumu ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kutafuta suluhisho na kulichukulia suala la maadili kwa uwazi ndani ya jamii.
“Kuwakutanisha Wahariri na vyanzo vya taarifa na elimu ambao ni viongozi wa Dini na Wadau wengine katika kikao hiki kitatupa fursa ya kwenda mbele zaidi kwani jukumu letu kuhakikisha tunapohabarisha tunaufahamu na kitu hicho. Umetujengea mahusiano na watoa taarifa” amesema Bakari Machumu.
Kwa upande wake Mchungaji mstaafu na Mkurugenzi wa Taasisi ya Hananja Compassion Foundation, Richard Hananja amesema majadiliano hayo yamekuja kwa wakati muafaka kutafuta suluhisho la changamoto ya maadili katika jamii.
“Watu wanakwenda kwenye nyumba za Ibada, tutumie nyumba za ibada hasa kwa Waumini wa Dini na Madhehebu mbalimbali kutoa elimu ya maadili kwa jamii” amesema Mchungaji Hananja.
Naye Shekh Rashid Shemzigwa aliyezungumza kwa niaba wa shekh wa mkoa wa Dar es Salaam, amesema kuwe na muda wa kutosha wa kujadili masuala ya maadili kwa Wadau wote Ili kuhakikisha changamoto ya mmomonyoko wa maadili inahubiriwa kila mahali.
Akifungua kikao hicho Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima amebainisha kuwa lengo la kikao hicho ni kuhakikisha ajenda ya maadili inamilikiwa na jamii yenyewe Ili kurudi kwenye utamaduni uliokuwepo hapo awali.
“Mfano nenda kwenye mikutano ya jamii ukauliza vipaumbele ni nini, utasikia afya, maji, elimu, umeme, barabara, kilimo, mifugo na vitu kama hivyo, nadra sana kusikia mmomonyoko wa maadili kuwa ni kipaumbele chetu. Bado umiliki wa hili jambo tunatakiwa tuupeleke kwenye meza zote za maamuzi sekta zote” amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Ameelezea Tamasha la kutangaza fursa za kiuchumi kwa kushirikiana na Wadau litakalozinduliwa Aprili 27-29, 2023 mkoani hapa mwelekeo wake ni kumilikisha ajenda ya maadili kwa wananchi na kuwaelimisha wananchi juu ya fursa za kiuchumi. Aidha, amewashukuru Taasisi ya FAGDI kwa kujitoa kuandaa tamasha hili pamoja na wadau wote waliochangia kuwezesha, amewashukuru SMAUJATA na wengine wengi wanaoendelea kujitokeza kuichukua ajenda hiyo.
Awali, akiwasilisha mada kwa washiriki, Mtaalamu wa Saikolojia Dkt. Chris Mauki amewakumbusha wazazi kutotumia muda mwingi kutafuta fedha Ili kuwarithisha watoto wao badala ya kuwarithisha tabia njema yatakayosaidia kuwa na jamii yenye maadili mema .