Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameshuhudia utiaji Saini wa Makubaliano hayo uliofanyika leo Aprili, 24, 2023 jijini Dodoma ambapo amesema makubaliano hayo yatasaidia kuibua fursa kwa wadau wa Filamu kupata mafunzo kuhusu namna ya kutengeneza Filamu bora zitakazopata nafasi katika soko la ndani na nje ya Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mashirikiano ya Kimataifa (BFIC) kutoka nchini Korea Kusini Bw. Chi Lee akizungumza jambo leo jijini Dodoma.
……………
Tanzania kupitia Bodi ya Filamu imesaini Mkataba wa Makubaliano ya Ushrikiano na Taasisi ya Mashirikiano ya Kimataifa (BFIC) kutoka nchini Korea Kusini kwa ajili ya uendelezaji wa tasnia ya Filamu hapa nchini katika eneo la uandaaji na utengenezaji wa filamu bora.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameshuhudia utiaji Saini wa Makubaliano hayo uliofanyika leo Aprili, 24, 2023 jijini Dodoma ambapo amesema makubaliano hayo yatasaidia kuibua fursa kwa wadau wa Filamu kupata mafunzo kuhusu namna ya kutengeneza Filamu bora zitakazopata nafasi katika soko la ndani na nje ya Tanzania.
“Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwenye sekta zetu. Tanzania sasa ni ya pili katika Sekta ya filamu ikitanguliwa na Nigeria, kwa siku inazalisha filamu nne. Kupitia makubaliano haya, tutaongeza Idadi na filamu zetu zitakua na ubora zaidi kuliko ilivyo sasa kutokana na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uandaaji ” Amesisitiza Mhe. Balozi Pindi Chana.
Amewataka waaandaji wa Filamu nchini Tanzania watengeneze Filamu zinazozingatia maadili ya Kitanzania ambazo zinatangaza Utamaduni na lugha ya Kiswahili ili Dunia izidi kuifahamu Tanzania.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu kutoka Taasisi hiyo Bw. Chi Lee ameeleza kuwa Taasisi hiyo ipo tayari kuisaidia Tanzania katika Sekta ya filamu kwa kutoa Wataalam watakaosaidia kutoa mafunzo kwa waandaaji na waigizaji wa Filamu nchini Tanzania.
Aidha, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo ameeleza kuwa makubaliano hayo ni mafanikio yaliyotokana na ushirikiano mzuri baina ya Tanzania na Korea Kusini ambayo imeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa ubora wa tasnia ya filamu nchini.