Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Fatma Mwasa (kushoto) akimkabidhi zawadi mmoja wa wanafunzi wanaofanya vizuri darasani kwenye kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yaliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mvuha, mkoani Morogoro, katikati anayeshuhudia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Ms. Faraja Nyalandu.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Fatma Mwasa akihutubia wadau wa elimu kwenye hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yaliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mvuha, mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Ms. Faraja Nyalandu. akihutubia wadau wa elimu kwenye kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yaliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mvuha, mkoani Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Fatma Mwasa (kushoto) akimkabidhi zawadi mmoja wa wanafunzi wanaofanya vizuri darasani kwenye kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yaliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mvuha, mkoani Morogoro. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Ms. Faraja Nyalandu na Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga wakishuhudia.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Fatma Mwasa (kulia) akitembelea Banda la Shirika la CAMFED Tanzania kwenye hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yaliofanyika katika Kata ya Mvuha mkoani Morogoro, anayetoa maelezo kushoto ni Afisa Miradi ya CAMFED-Morogoro, Bi. Stumai Kaguna.
Maandamano ya wanafunzi na vijana wa skauti kwenye hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yaliofanyika katika Kata ya Mvuha mkoani Morogoro.
……………
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Fatma Mwasa juzi amefunga rasmi Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yaliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mvuha, mkoani Morogoro, huku akimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro kuhakikisha anazifanyia kazi changamoto za elimu zilizoibuliwa na wadau wa elimu katika maadhimisho hayo.
Akizungumza katika hafla hiyo Uwanja wa Shule ya Msingi Mvuha, Mhe. Mwasa alisema ili kukabiliana na changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu, serikali ya wilaya kuhakikisha suala la mahali pa kujenga kwa kuangalia ufikikaji kwa wanafunzi wote.
Alishauri shule zijengwe sehemu ambayo ni katikati na rahisi kufikika na wanafunzi wote na kwa shule ambazo zimejengwa tayari na zina msongamano ipo haja ya kuangalia uwezekano wa kujenga shule shikizi kwenye maeneo ya wanafunzi wanaotembea umbali mrefu hasa kwa watoto wa awali.
“…Nimeambiwa kuwa kuna mwamko mdogo wa wananchi katika kuendeleza elimu hapa kutokana na shughuli za kiuchumi kama kilimo na ufugaji ambavyo huathiri mahudhurio endelevu ya wanafunzi. Naagiza Mkuu wa wilaya na timu yako kuhakikisha wanafunzi wote walioandikishwa na wenye umri wa kwenda shule wanaenda shule na wazazi wasiotaka kuwasomesha watoto wao waelimishwe na wasiotaka kubadilika wachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Mhe. Mkuu wa Mkoa Mwasa.
Akizungumzia suala la utoro hasa kwa wasichana ambao wanaacha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za ufugaji, minada, vigodoro na ujauzito maeneo hayo alimuagiza Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Maafisa Elimu kuvikomesha kabisa vitendo hivyo.
“Na kama wasichana waliokatiza masomo na uwezo wa kuendelea na taaluma wasaidiwe kurudi shule na kumalizia masomo yao. Kuna suala la mila na desturi potofu zinazowanyima fursa watoto wote wa kike na wa kiume kupata elimu kama vile kuwaozesha watoto mapema na kuwacheza ngoma watoto wa kike.
Katika haya niliyoyataja tunahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi na viongozi wa ngazi zote kuanzia viongozi wa Vitogoji/mitaa, vijiji na kata, viongozi wa kimila, viongozi wa dini na wananchi wote kwa ujumla ili kutokomeza mila hizi potofu; na atayekwamisha jitihada hizi serikali haitasita kumchukulia hatua kali,” alisisitiza Mhe. Mwasa.
Akizungumza awali akihutubia washiriki wa Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa, Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Ms. Faraja Nyalandu aliishauri Serikali kwa kushirikiana na jamii pamoja na wadau wengine kuwekeza katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, majengo ya utawala, matundu ya vyoo na vyumba maalum kwa watoto wa kike pindi wanapokuwa kwenye hedhi changamoto ambayo imeibuliwa na wadau.
Aliitaka Jamii kuendelee kuhamasishwa kuchangia huduma ya chakula na lishe bora, maji safi na salama shuleni, Walimu kushirikiana na kamati za shule, bodi za shule, serikali za vijiji, wazazi, na wanajamii kuweka mikakati ya pamoja kudhibiti suala la utoro shuleni na kuendelea kueliemishwa juu ya mila zinazo athiri ushiriki wa wanafunzi kupata elimu bora.
Aidha aliiomba Serilkali kuendelea kuajiri walimu ili kupata uwiano kati ya idadi ya mwalimu na wanafunzi, Pia iajiri walimu wa elimu maalum pamoja na wasaidizi wao na wazazi kuendelea kuelimishwa juu ya umuhimu wa kuwaandikisha watoto wenye ulemavu shuleni.
“…Serikali kwa kushrikiana na wadau wa elimu iendelee kutoa vifaa vya kujifunza na kujifunzia ikiwemo vitabu na vifaa vya mahabara, jamii na wadau waanzishe vituo shikizi hasa kwa watoto wa madarasa ya awali hadi darasa la tatu pamoja na jamii kuhamasishwa kuanzisha na kuendesha vituo vya kulelea watoto wadogo mchana (Community Based ECD Centers),” aliongeza Mwenyekiti huyo wa Bodi ya TEN/MET.
Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yaliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mvuha, mkoani Morogoro, yalizinduliwa na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mh. Rebeca Nsemwa mnamo tarehe 17 Aprili 17, 2023 na kufungwa na Mheshimiwa Fatma Mwasa Mkuu wa mkoa wa Morogoro Aprili 21, 2023.