Afisa Miradi ya CAMFED-Morogoro, Bi. Stumai Kaguna (kulia) akitoa elimu ya stadi za maisha kwa baadhi ya wanafunzi walioshiriki katika juma ili kuwajengea uwezo ili kutambua changamoto zao na namna ya kukabiliana nazo. |
Na Joachim Mushi, Mvuha-Morogoro
SHIRIKA la CAMFED limetumia Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yaliofanyika katika Kata ya Mvuha mkoani Morogoro, kutoa elimu ya stadi za maisha kwa wanafunzi walioshiriki katika juma ili kuwajengea uwezo ili kutambua changamoto zao na namna ya kukabiliana nazo.
Akitoa elimu hiyo kwa makundi ya wanafunzi katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mvuha, Afisa Miradi ya CAMFED-Morogoro, Bi. Stumai Kaguna alisema elimu ya stadi za maisha walioitoa kwa wanafunzi hao inawasaidia kutatua changamoto anuai wanazokumbana nazo wakiwa mazingira ya shuleni na hata nje ya shule.
Alisema programu hiyo pia imesaidia kupunguza utoro shuleni kwa wanafunzi na kuwasaidia kuongeza ufaulu katika masomo yao, programu ya Stadi za Maisha au Dunia Yangu Bora inalengo la kuhakikisha inawasaidia wanafunzi wa kike na kiume kwanza kutambua changamoto zao, na namna ya kuzitatua changamoto hizo.
“Kupitia programu hii, watoto wa kike pamoja na wavulana wanajifunza mada mbalimbali ambazo zinawafanya wao waweze kujitambua, kutambua changamoto zao wanazokumbana nazo katika mazingira ya kila siku.
Pia kuweza kuona ni namna gani wanaweza kutambua changamoto hizo, hivyo zipo mada mbalimbali kama; mada za ustawi, mada za uwezo…mada za kujitambua, kujiamini kuwa jasiri na mtoto anapokuwa jasiri na anayejitambua anaweza kushughulikia changamoto zake,” alisema Bi. Kaguna akizungumzia programu hiyo kwa wanahabari.
Aidha aliongeza kuwa mtoto anapokuwa jasiri na mwenye uwezo wa kujitambua anapokutana na changamoto yoyote anaweza kusimama imara na kufanya uamuzi sahihi katika kutatua changamoto yake na hatimaye kutimiza ndoto zake kimaisha.
Akifafanua zaidi juu ya programu hiyo, alibainisha kuwa kwa mkoani Morogoro inatekelezwa katika Wilaya saba, ndani ya shule 28 zinazo nufaika na Programu ya Dunia Yangu Bora, huku wawezeshaji wa programu wakiwa ni wasichana ambao ni wanufaika wa programu za CAMFED kutoka maeneo mbalimbali ya kata zilipo Sekondari zenye mradi huo.
“Kwa mkoa wa Morogoro tunafanya kazi katika Wilaya za Kilosa, Wilaya ya Gairo, Wilaya ya Mvomero, Wilaya ya Ifakara, Wilaya ya Mlimba pamoja na Wilaya ya Ulanga,” alisisitiza Afisa Miradi huyo wa CAMFED-Morogoro, Bi. Kaguna akizungumza na wanahabari.