Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo na Naibu Waziri Mhe. Khamis Hamza Khamis wakipongezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 leo Aprili 24, 2023.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo Akitoa maelezo kuhusu hoja za wabunge zilizojitokeza wakati wa kujadili hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 aliyoiwasilisha bungeni leo Aprili 24, 2023.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akipongezwa na wabunge mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 leo Aprili 24, 2023.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis (katikati) akifurahia jambo na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga (kushoto) pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji, na Mazingira Mhe. Jasckson Kiswaga mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 leo Aprili 24, 2023.
……….
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Aprili 24, 2023 limepitisha Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 kiasi cha ya Sh. 54,102,084,000 kwa matumizi mbalimbali yakiwemo miradi ya maendeleo.
Akitoa maelezo kuhusu hoja za wabunge zilizojitokeza wakati wa kujadili hotuba hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali itaendelea kuhakikisha inatenga bajeti ya kutosha kuweza kutekeleza miradi ya hifadhi ya mazingira.
Dkt. Jafo Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na jukumu la kuratibu suala la usimamizi na hifadhi ya mazingira kazi inashirikiana na wizara za kisekta katika kusukuma mbele ajenda ya mazingira.
“Mheshimiwa Naibu Spika ni kweli bajeti imekuwa haitoshi kama ambavyo kamati na wabunge walivyochanga lakini jukumu letu kubwa ni kuhakikisha tunatekeleza miradi ili isaidie karika kulinda mazingira kwa mfano tumechimba malambo katika maeneo kame yote haya ni kuhakikisha wananchi wanakabiliana na athari za kimazingira,” amesema.
Akiendelea kujibu hoja za wabunge waliochangia hotuba hiyo pia, Waziri Jafo amesema kuwa hivi sasa wananchi wanahamasishwa katika kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti ili kunufaika na Biashara ya Kaboni.
Amesema hivi sasa Halmashauri Tanganyika imeweza kuingiza mabilioni ya fedha kutokana na kuhifadhi misitu na hivyo hatua hiyo itasaidia kuhamasisha wananchi waendelee kupanda miti.
“Biashara ya Kaboni inafungua milango ya uwekezaji ndio maana Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa Mwongozo na Kanuni na kutokana na hatua hiyo sasa tunafungua mlango mpana wa upatikanaji wa fedha kupitia biashara hiyo,” amesema.
Awali akichangia hoja, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha viwanda vinadhibiti uchafuzi wa mazingira.
Amesema viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais wamekuwa wakitoa maelekezo kwa wenye viwanda wahakikishe wanatengeneza mifumo ya kuzuia majitaka yasitiririke ovyo kwenye makazi pamoja na moshi usisambae ovyo hewani.