Timu ya Wizara ya Uchukuzi (waliovaa jenzi ya njano) ya mpira wa wavu wanaume
wakimenyana na timu ya Wizara ya Maliasili (jezi ya bluu) wakati wa mashindano ya
Mei Mosi yanayoendelea mkoani Morogoro.
Timu ya Mahakama (waliovaa jenzi nyekundu) ya mpira wa netiboli wakimenyana
na timu ya Wizara ya Maliasili wakati wa mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea
mkoani Morogoro.
Timu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) (waliovaa jenzi ya kijani) ya mpira
wa wavu wanawake wakimenyana na timu ya Morogoro DC (jezi nyekundu) wakati wa
mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea mkoani Morogoro.
Julius Magige (katikati) wa timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akichanja
mbuga kuelekea golini huku walinzi Romanus Mkude (kushoto) na Zakayo
Mtungalyambo (kulia) wa timu ya RAS Dodoma wakihakikisha haleti madhara kwenye
lango lao katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi iliyofanyika kwenye
uwanja wa Morogoro Sekondari.
………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
TIMU za Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa zimejihakikishia
kucheza hatua ya 16 bora kwa mchezo wa soka katika mashindano ya Kombe la Mei
Mosi inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali mkoani Morogoro baada ya kujikusanyia
alama nyingi kwenye makundi yao.
TAMISEMI ambayo ipo kundi A imejikusanyia alama 10, huku TRA waliopo kundi B
wanapointi 11 na Ulinzi waliopo kundi C wanapointi tisa. Timu nyingine zinazoungana
na hizo za kundi A ni Mahakama, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari na Wizara ya Afya.
Zilizopo kundi B ni Benki ya CRDB, Shirika la Maendeleo ya Petrol (TPDC) na Wakala
wa Barabara Tanzania (TANROADS), kundi C zipo Hazina, Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Mambo ya Ndani; huku za kundi C
zipo Wizara ya Maliasili na Utalii, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wizara ya
Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) na Morogoro DC.
Katika hatua nyingine timu ya Moro DC leo imeona mwezi baada ya kuifunga Ukaguzi
kwa magoli 4-0; huku 21 Century waliwachapa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa 3-
0; nao Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa waliwashinda Wizara ya Mambo ya
Ndani kwa 3-1; nayo Mahakama waliwaadhibu Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Taifa
(NFRA) kwa magoli 3-1; na Benki ya CRDB waliwashinda Chuo Kikuu cha Kilimo cha
Sokoine (SUA) kwa 2-1; wakati zilizotoka sare ni Sekta ya Uchukuzi na TANESCO (1-
1), Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na TAMISEMI (0-0); na
Hazina na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (0-0).
Katika mchezo wa netiboli Sekta ya Uchukuzi wamewafunga TRA (33-17); Halmashauri
Gairo imezinduka na kuwafunga Moro DC (34-9),Ulinzi wamewaadhibu TANROADS
(56-4); Wizara ya Afya waliwachapanga TPDC (33-20); Ofisi ya Rais Ikulu
waliwafindisha RAS Dodoma kwa 49-9; Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
waliwafunga waliwafunga Wizara ya Mambo ya Nje kwa 47-5 na Maliasili waliwaliza
Mahakama kwa 33-24.
Katika mchezo wa kuvuta kamba wanaume timu zilizoshinda kwa mivuto 2-0 na
matokeo yakiwa kwenye mabano ni Ofisi ya Rais Ikulu vs Mahakama; Wizara ya Kilimo
vs RAS Dodoma; TPDC vs Wizara ya Afya; Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari vs Tume ya Maendeleo ya Ushirika (2-0); huku Wizara ya Mambo ya Ndani vs
Maliasili na Utalii (1-1); kwa upande wa wanawake TPDC waliwavuta wenzao wa Tume
ya Maendeleo ya Ushirika kwa 2-0; huku Ofisi ya Waziri Mkuu Sera walitoshana nguvu
na Wizara ya Madini kwa 1-1.
Katika mchezo wa mpira wa wavu kwa wanaume timu ya Sekta ya Uchukuzi
waliwashinda Wizara ya Maliasili na Utalii kwa seti 2-0; nayo Moro DC waliwashinda
Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa seti 2-0; huku kwa wanawake TANESCO
waliibuka kidedea mbele ya Moro DC kwa 2-0; huku RAS Dodoma waliwashinda
Halmashauri ya Gairo kwa 2-1 na TANESCO tena waliwashinda jamaa zao wa TPDC
kwa 2-0.
Michuano hiyo itaendelea kesho kwa michezo mbalimbali itakayofanyika kwenye
viwanja vya Jamhuri, SUA Kampasi ya Mazimbu, Tumbaku, Ujenzi na Moro Sec.