Na. Damian Kunambi, Njombe
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva akiwa sambamba na mashekhe wa wilaya ya Ludewa wametembelea wodi ya wakina mama waliojifungua na wanaosubiri kujifungua katika hospitali ya wilaya hiyo na kuonyesha upendo kwa kuwapa vitu mbalimbali wakina mama hao.
Akizungumza mara baada ya kuwasili hospitalini hapo mkuu huyo wa wilaya akiwa na shekhe wa wilaya Haruna Rahimu, shekhe Ismail Kanju pamoja na watumishi mbalimbali kutoka katika wilayani na madaktari amesema wameona ni vyema kujumuika na viongozi hao wa dini ikiwa ni njia mojawapo ya kufanya matendo ya huruma na kujenga imani ya kidini na wakaona ni vyema kuonyesha upendo wao kwa kuwatembelea wakinamama hao wajawazito na wanaosubiri kujifungua.
“Nimewaletea salamu kutoka kwa Rais wetu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan rais ambaye anaupendo kwa akina mama na watoto pia hivyo mimi pamoja na mashekhe hawa katika kipindi hiki cha ramadhani tumekuja kuwapa salamu za upendo kutoka kwa rais wetu Dkt. Samia”
Aidha kwa upande wake shekhe wa wilaya Haruna Rahim wamewaasa waumini wote wa kiislam hapa nchini kukumbuka kutoa zaka katika kipindi hiki cha ramadhani kwakuwa kipindi hiki kinahusiana na matendo ya huruma, pamoja na kujifunza mambo ikiwemo kutoa zaka kwa watu wa makundi mbalimbali.
Wakina mama hao wamepatiwa vitu mbalimbali ikiwemo sabuni, mafuta ya kupaka watoto, dawa za meno na miswaki, pamoja na pampas.


