Na Beatrice Sanga-MAELEZO
SERIKALI imesema kuwa itahakikisha Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyopo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina yanajiendesha kwa faida katika shughuli zake na kuchangia ukuaji wa pato la taifa kwa kutoa gawio, lengo likiwa kuleta tija kwa uchumi wa nchi na pia kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu.
Hayo yameelezwa Jijini Dar es
Salaam Aprili 19, 2023.na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu wakati wa Mkutano kati yake na Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali, uliolenga kuweka mikakati ya namna ya kusimamia mashirika hayo kujiendesha kibiashara.
“Mashirika mengi yanayoweza kutoa huduma yanapaswa kuingia kwenye biashara, lazima tubadili uwezo wetu wa kufikiri kibiashara, namna gani ya kutumia rasilimali ili kupunguza utegemezi kutoka serikalini na kujitegemea,” Ameeleza Mchechu.
Mchechu amesema kuwa mkutano huo una lengo la kuwakumbusha viongozi, wa Mashirika ya Umma na Taasisi mbalimbali majukumu ya ofisi yake na mipango yake ya kuhakikisha kwamba kila mmoja anatekeleza wajibu wake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Sheria na kusimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya Watanzania wote.
“Wanatakiwa wajue Serikali ina matarajio na nia ya kuongeza ufanisi katika mashirika ya umma, tunategemea baada ya haya tutakuwa na utendaji kazi wa karibu zaidi, tutakuwa na ufanisi na tunapokuwa na ufanisi maana yake ni mapato ya Serikali nayo yanakwenda kuongezeka kwa maana ya kuchangia kwenye gawio, lakini pia taasisi hizi zinapofanya vizuri ajira na huduma zake zinazidi kutalamaki,” Amesema Mchechu.
Akizungumza juu ya Mashirika ambayo yanayopaswa kufutwa ama kuunganishwa ili kuongeza ufanisi kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan wakati akipokea Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali hivi karibuni, Mchechu amesema kuwa bado Serikali inapitia na kuangalia kama itayabadilisha ama kuyaunganisha na kila kitu kitakapokamilika taarifa rasmi itatolewa.
“Kwa sasa tunaangalia changamoto kwamba kwanini kwa sasa mashirika hayatoi gawio wakati labda changamoto ni mitaji kuna wengine hawana uongozi imara na kama uongozi siyo imara tunakukumbusha na kama haukumbushiki tutafanya mabadiliko,” amesisitiza Mchechu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa amesema kuwa, Mashirika ya umma yanapaswa kusimamia uzalishaji na uendeshaji wa mashirika hayo kwa faida, na kuhakikisha kuwa yanachangia katika mfuko mkuu wa hazina kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
“Mfano kwa upande wetu TRC tuna kazi ya kutoa huduma kwa watu, lakini pia tunasafirisha mizigo, mizigo kwa sehemu kubwa ni biashara, biashara yetu iko kwenye mizigo, kwa watu ni huduma zaidi ndo maana gharama zetu ni ndogo sana kwa kwa upande wa mizigo kule ndo tunatengeneza biashara kwa hiyo tuna majukumu hayo ya kuhakikisha kuwa tunatengeneza pesa na kutoa gawio,” ameeleza Kadogosa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo amesema kuwa ujio wa Msajili wa Hazina itakuwa ni chachu kubwa kutokana na mipango ambayo amekuja nayo hususani katika kusisitiza mashirika na taasisi kujikita katika uzalishaji zaidi kuliko kutoa huduma pekee.
“Sasa hivi mashirika yetu yana baadhi ya changamoto ambazo zilikuwa hazijapatiwa nafasi ya kuzizungumza, lakini tumefurahi kuona kwamba Msajili wa Hazina baada ya kuteuliwa tayari amejipanga hata kabla hajakutana na sisi kufanya mabadiliko, na mabadiliko aliyoyasema kwa kweli yanakwenda kuyafanya mashirika haya yawe kwenye nafasi nzuri ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.”
Katika mkutano huo, mbali na hayo Mchechu amesema kuwa kwa sasa Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia mashirika 298, wakati huo mashirika 35 yanajihusisha na biashara, ilhali Mashirika 213 yanajihusisha na utoaji wa huduma, na mpaka sasa Serikali imewekeza zaidi ya Sh. Trilioni 70 katika mashirika haya na imekuwa ikitegemea kupata gawio kutoka katika mashirika, ingawa kumekuwa na kulegelega katika kujiendesha huku mengine yakikabiliwa na ukosefu wa mitaji na kujiendesha kwa hasara.
Hata hivyo, kutokana na mipango inayofanya na Ofisi ya Msajili wa Hazina sasa wanatarajia kuwa mashirika mengi yatakwenda kujiendesha kwa faida kuliko kuhudumiwa zaidi na Serikali pekee.
Vikao hivyo kati ya Msajili wa Hazina na Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali vinatarajiwa kuhitimishwa kesho Alhamisi kwa Msajili kukutana na taasisi na mashiriki zaidi ya 170 yasiyofanya biashara