Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
April 19
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira,alhaj dkt.Seleman Jafo amesisitiza matumizi ya Nishati mbadala katika Taasisi za umma na binafsi zenye watu zaidi ya 100 ,ili kuokoa gharama kubwa zinazotumika katika manunuzi ya mkaa na kuni.
Aidha amehimiza wananchi kuungana katika Utunzaji na kulinda Mazingira ili kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaathiri Mazingira na Uchumi.
Jafo alitoa msisitizo huo , April 19 wakati akizindua kampeni ya Mazingira na matumizi ya Nishati mbadala pamoja na mashindano ya upandaji miti ,uliofanyika shule ya Sekondari ya wasichana Ruvu ,Kibaha Vijijini Mkoani Pwani,ambayo imeandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani.
Alieleza lengo kubwa ni kusonga mbele katika kudhibiti uharibifu wa Mazingira,ukataji miti ambapo Serikali ilishatoa tamko Taasisi hizo kujikita na matumizi ya Nishati mbadala na maelekezo hayo hayakugusa mwananchi mmoja mmoja licha ya kwamba wananchi wanatakiwa kutunza Mazingira na kuacha kukata miti ovyo.
“Niwapongeze Taifa gas kwa kuwafungia mtungi wa gas wa milioni sita katika shule ya Sekondari ya wasichana Ruvu kwa ajili ya matumizi ya jiko la shule hii”na Leo huu ni ushuhuda tosha kuona kwamba mambo haya yanawezekana.”
Kama Sekondari zote zikiweka Utaratibu na Taifa gas kuweza kufungiwa gas shule zote za bweni ,zitatumia Nishati mbadala na kuweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha,:;”anafafanua Jafo.
Hata hivyo ,Jafo alieleza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kujipambanua katika suala zima la Mazingira ,na kuwa na miradi ya kujali Mazingira.
Akitoa salamu za mkoa , Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Pwani,mkuu wa wilaya ya Kibaha Nikkison Simon alisema ,mkoa huo una changamoto kubwa ya kimazingira hivyo wameamua kujipambanua katika upande wa mazingira ili kupambana na hali hiyo.
Alieleza, mkoa umeshapanda miti milioni Tisa sawa na asilimia 82 ,lengo likiwa kupanda miti zaidi ya milioni 13.
Vilevile ,wamejipanga kuongeza usimamizi wa mazingira, upandaji miti, teknolojia mbadala na uchumi.
Kwa upande wa Taifa Gas ,Angella Bhoke alielezea kuwa, wanajenga kiwanda Cha mitungi ya gas Misugusugu lengo ni kushirikiana na Serikali katika kudhibiti uharibifu wa Mazingira na kuhimiza matumizi ya Nishati mbadala.
Katika shughuli hiyo wamegawa mitungi 300 kwa makundi mbalimbali,na wameandaa mashindano ikiwemo kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari ambao watajikita kutoa elimu ya Nishati mbadala na kudhibiti uharibifu wa Mazingira,anasema Angella.
Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Dar es salaam ,Seko Urio alieleza , wamejipanga kupanda miti milioni moja kwa mwaka ,katika uzinduzi huo wamepanda miti 250.
Alibainisha, kwasasa wanaendelea na Zoezi la kampeni ya kuza mti Tukutunze ambapo wametenga milioni 472 kwa ajili ya kushindanisha shule zote nchini kupanda miti na kuhakikisha inakua.