Mtafiti msaidizi wa Mambo ya kale kutoka Makumbusho ya Taifa Adson Ndyanabo akizungumza na mwandishi wa habari hizi ikiwa ni katika kuadhimisha siku ya Malikale au urithi Duniani ambayo huadhimishwa April 14 ya kila mwaka.
………………….
NA MUSSA KHALID
Watanzania wametakiwa kushiriki kwa pamoja kutunza, kuchangia na kukuza Malikale mbalimbali zizilizopo nchini kwani ni muhimu kwa kizazi cha sasa na baadae.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mtafiti msaidizi wa Mambo ya kale kutoka Makumbusho ya Taifa Adson Ndyanabo wakati akizungumza na Kituo hiki ikiwa ni katika kuadhimisha siku ya Malikale au urithi Duniani ambayo huadhimishwa April 14 ya kila mwaka.
Amesema siku hiyo ilianza kutambulika na UNESCO katika mkakati wa kuifanya kuwa rasmi mwaka 1964 lakini ilipofika April 18 ,1982 Baraza la Usimamizi wa Malikali Kimataifa ilipendekeza siku hiyo kuthibitishwa rasmi mwaka mmoja baadae.
Amesema malengo ni kuhakikisha kwamba jamii inapata uelewa kuhusiana na Malikale kwani zimekuwa ni sehemu ya kuelezea utamaduni na teknolojia ya mwanadamu toka alipo na anapokwenda.
‘Hizi Malikale nyingi zinakuwa na muda wake kitaalamu licha kuwa zinatakiwa kuwa na muda lakini zinatakiwa kuwa nathamani maalum na kigezo ni umri hivyo katika kuhakikisha tunazilinda ndio maana ikatengwa hii siku maalum’amesema Ndyanabo
Amesema nchi imesheheni Malikale mbalimbali zikiwemo zilizopo katika Pwani ambazo zinaelezea historia ya mwingiliano kati yetu na watu kutoka bara la Asia.
‘Ukizungumzia Maeneo kama Mji wa Dar es salaam kuna Malikale nyingi sana ukizungumzia Sanamu la Askari Posta,Old Boma na maeneo mbalimbali ikiwemo Kunduchi.
Kuhusu Jitihada wanazozifanya ili wananchi kufahamu uwepo wa Malikale hizo Ndyanabo amesema wamekuwa wakifanya uhamasishaji kupitia vyombo vya habari na Matamasha mbalimbali ili kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kuhifadhi Malikale hizo.
Amesema kupitia filamu ya Royal Tour ambayo imechezwa na Rais Dkt Samia Suluh Hassan imesaidia kuhamasisha na kutembelea vituo vya kiutalii ambavyo vimekuwa na kumbukumbu nzuri ya Kihistoria ya kuhusu maisha ya watangulizi wa Taifa.
Suala la kutambua maana na umuhimu wa malikale kwa jamii siyo jambo geni kwa Watanzania. Tangu enzi za wahenga wetu, kabla Wazungu hawajaingilia uendeshaji wa utawala na utamaduni wa jamii zetu, wakazi wa Tanzania na kwingineko duniani walikuwa wanaenzi na kuhifadhi vitu vya kale vilivyokuwa vimejipatia umuhimu fulani kutokana na mchango wake katika jamii husika.