……………
Na Mwandishi Wetu, Musoma
Shirika la Nyumba la Taifa limekabidhiwa rasmi Jengo la kisasa la Biashara la Mukendo Commercial Complex mjini Musoma Mkoani Mara kutoka kwa Mkandarasi aliyetekeleza ujenzi wake Kiure Engineering Limited.
Wataalamu wa ujenzi pamoja na wawakilishi wa Shirika la Nyumba la Taifa na wale kutoka katika Kampuni ya Ujenzi ya Kiure Engineering wamekabidhiana leo rasmi jengo hilo la awamu ya pili baada ya kukamilisha ujenzi huo uliodumu kwa miaka mitatu.
Akikabidhi jengo hilo, Mhandisi Juma Mkwawa amesema Kampuni yake kwa kushrikiana na Shirika la Nyumba la Taifa imeitia orodha yote ya marekebisho na maboresho yaliyotakiwa kufanywa na Mkandarasi na wamejiridhisha kuwa kazi hiyo imekamilika.
Mkwawa amesema Kampuni yake imetekeleza mradi huo wa jengo lillojengwa kwa awamu kwa ustadi mkubwa na kuwezesha kukamilisha jengo hilo ambalo sasa linatumika na wateja mbalimbali.
Naye Mhandisi Mburuga Matamwe amesema kuwa wameridhishwa na ukamilishwaji wa jengo hilo na hasa baada ya kupitia orodha ya mambo yote muhimu yaliyotakiwa kuboreshwa na kwamba sasa wanalikabidhi jengo kwa Meneja wa NHC Mkoa wa Mara.
Kaimu Meneja wa NHC Mkoa wa Mara, Joseph John amesema kwamba wameridhishwa na ukamilisho uliofanywa na mkandarasi na kwamba sasa wanawakaribisha wateja mbalimbali kufika kupanga katika jengo hilo.
Amewakaribisha Watanzania wote na wenyeji wa Mkoa wa Mara kuchagamkia fursa za upangaji katika jengo hilo kwa kuwa ni jengo bora Musoma nzima.
Mji wa Musoma umepata muonekano mpya kwa kuongezewa jengo refu, kubwa na la kisasa kwa shughuli za kiosifi na biashara. Lenye huduma huduma zote muhimu yakiwamo maeneo ya benki, Biashara na Ofisi mbalimbali za kisasa.