Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Sekta ya Ujenzi (hawapo pichani), wakati akifungua baraza hilo, jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akisisitiza jambo kwa Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekta ya Ujenzi (hawapo pichani), wakati akifungua baraza hilo, jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Sekta ya Ujenzi, ambaye ni Katibu Mkuu-Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, akizungumza na wajumbe wa baraza (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa baraza la wafanyakazi Sekta ya Ujenzi, lililofanyika Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wa Sekta ya Ujenzi, wakimsikiliza mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa baraza la wafanyakazi, lililofanyika Jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa baraza la wafanyakazi Sekta hiyo, mara baada ya kufungua baraza la Sekta ya Ujenzi, Jijini Dodoma.
PICHA NA WUU
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amewataka watendaji wa Sekta ya ujenzi kuhakikisha wanafuatilia na kusimamia miradi ya ujenzi inayotekelezwa ili kukamilika kwa wakati na kuwa na tija kwa wananchi.
Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi na kusisitiza kuwa ufuatiliaji huo utasababisha miradi inayotekelezwa kulingana na thamani ya fedha iweze kuleta matokeo chanya na kuweza kukamilika kwa wakati.
“Napenda kuwakumbusha wajumbe kuwa mnatakiwa kuendelea kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kusimamia utekelezaji wa Miradi mbalimbali katika sekta ya ujenzi ikiwemo Barabara, Madaraja na Vivuko.” amesema Profesa Mbarawa.
Aidha,Waziri Mbarawa amewatahadharisha watumishi wa Sekta hiyo kujiepusha na matumizi mabaya ya madaraka pamoja na ubadhirifu wa mali za umma, hali ambayo italeta taswira mbaya kwa taasisi na Wizara kwa ujumla.
Pia, ametoa rai kwa wajumbe wa baraza hilo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi, maarifa, uadilifu na uzalendo wa hali ya juu, utakaosababisha kufanikisha maendeleo ya taasisi na Serikali kwa ujumla.
Waziri Mbarawa amefafanua kuwa katika hatua ya kuongeza ufanisi na utoaji wa huduma, Watumishi wanatakiwa wapewe maeneo mahsusi ya kufanyia kazi, hali itakayosaidia kupima utendaji wa watumishi, kuwakuza, kuwapa morari ya kazi na kuwawezesha kuwa wabunifu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, amemhakikishia Waziri Mbarawa, kuwa Sekta ya Ujenzi itaendelea kutekeleza majukumu yake katika kuchangia maendeleo ya Taifa na kuzingatia viwango vya ubora wa ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja, nyumba za Serikali na Vivuko pamoja na Ujenzi na Upanuzi wa Viwanja vya ndege.
Kuhusu Maslahi ya watumishi wa sekta hiyo, Katibu Mkuu huyo amesema kuwa Wizara itaendelea kulipa mishahara na kuwasilisha michango ya watumishi kwenye mfuko wa umma, (PSSSF) kwa wakati.
Mkutano huo wa Baraza ambao unafanyika kwa majibu wa Ibara ya 7 na 20 ya agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970 , umewashirikisha wajumbe ambao ni wakuu wa Idara na vitengo vya Sekta, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, Wajumbe wa Halmashauri ya tawi la TUGHE (Sekta ya Ujenzi) pamoja na wawakilishi wa idara na vitengo na wafanyakazi kutoka katika Taasisi zote zilizo chini ya Wizara kwa lengo mahsusi la kujadili na kuridhia Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24 kabla ya kuwasilishwa Bungeni.