Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso amefika wilayani Korogwe mkoa wa Tanga na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe Jokate Mwegelo kwa Ziara ya kikazi akiwa na lengo la kutatua changamoto mbalimbali na kufuatilia hali ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji na hali ya utoaji wa huduma ya Maji eneo la Korogwe mjini.
Akiwa wilayani Korogwe Waziri Aweso amefanya maamuzi ya kumuondoa kwenye nafasi yake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji ya Korogwe Sifael Masawa na kumuelekeza Katibu Mkuu Wa Wizara ya Maji Eng Nadhifa Kemikimba kuwa Mkurugenzi Sifael Masawa apewe nafasi kwenda kusoma ili kuongeza elimu na ufanisi katika utaalamu wa maswala ya Maji.
Pia ameelekeza Mamlaka ya Maji Korogwe kuwa chini ya uangalizi kwa Mhandisi Yohana Mgaza ambae anasimamia mradi wa Maji wa Kimkakati wa kitaifa wa HTM Korogwe-Habdeni.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso ameelekeza kuondolewa kwa Mkandarasi anaetekeleza mradi wa Maji wa Goha-Mkumbala Korogwe vijijini kutokana na kusuasua kumaliza utekelezaji wa Mradi huo na kazi isiorudhisha.
Mwisho amewaahidi wana Korogwe kuwa Wizara ya Maji inakwenda kusimamia kwa ukaribu kuhakikisha changamoto ya Maji Korogwe inabaki kuwa historia.