Afisa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Raphael Nemes akifafanua jambo kwa wakazi wa Vijiji vya Songambele na Kapalamsenga vilivyopo katika Kata ya Kaparamsenga, Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi waliohudhuria semina ya uhamasishaji iliyodhamiria kujenga uelewa wa pamoja ili kufanikisha zoezi la upangaji, upimaji na umilikishaji katika maeneo yao.
Afisa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Raphael Nemes akitoa elimu kwa wananchi waliohudhuria semina iliyolenga kujenga uelewa wa pamoja ili kufanikisha zoezi la upangaji, upimaji na umilikishaji katika katika vijiji vya Songambele na Kapalamsenga vilivyopo katika Kata ya Kaparamsenga, Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.
Mwananchi kutoka Kijiji Cha Songambele akichangia mada wakati wa semina iliyolenga kujenga uelewa wa pamoja ili kufanikisha zoezi la upangaji, upimaji na umilikishaji katika katika vijiji vya Songambele na Kapalamsenga vilivyopo katika Kata ya Kaparamsenga, Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.
……………………………….
Na Magreth Lyimo, WANMM
Wakazi wa Vijiji vya Songambele na Kapalamsenga vilivyopo Kata ya Kaparamsenga, Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi wamehakikishiwa kuwa, lengo la Mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi (LTIP) ni kuwawezesha kumiliki maeneo yao Kisheria.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Afisa Mipango Miji Bw. Raphael Nemes wakati wa utekelezaji wa zoezi la uhamasishaji na utoaji elimu kwa wakazi wa vijiji viwili vya Songambele na Kapalamsenga vilivyopo katika Kata ya Kaparamsenga, Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.
Bw. Nemes alisema kuwa, lengo la mradi huo sio kuwanyang’anya au kopora ardhi kutoka kwa Wananchi bali ni kuyaongezea maeneo yao thamani ili waweze kuyamiliki kisheria.
Katika uhamasishaji huo, Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Tanganyika Bw. Mussa Segeja aliwaeleza wakazi wa Vijiji hivyo umuhimu wa kuacha nafasi kwa ajili ya kupitisha barabara kwenye mitaa yao jambo alilolieleza kuwa litarahisisha ufikishaji miundombinu muhimu kama vile umeme pamoja na maji katika maeneo yao.
“Wataalam watakapofika kuanza zoezi hilo tunawaomba msiweke ugumu kwenye kuacha nafasi kwa ajili ya kupitisha barabara, zitakazo wasaidia kurahisisha ufikaji wa mapema wa huduma za uokoaji kama vile zimamoto na kadhalika” aliongeza Segeja.
Naye Mtendaji wa Kata ya Kaparamsenga Bw. Paul Nyamuhanga aliwataka wananchi waliohudhuria mkutano huo kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa kuwafikishia taarifa majirani zao ili kuendelea kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa zoezi hilo.
Bw. Nyamuhanga aliwahimiza wananchi hao kuwepo katika maeneo yao wakati zoezi la upangaji litakapoanza ili kuondoa usumbufu wa kuingiliana kwa mipaka baina ya majirani waliopakana.
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi umejipanga kutoa hati za hakimilki za kimila 70,000 kwa wananchi ambapo awamu ya kwanza ifikapo Juni 2023 hati za hakimiliki za kimila takriban 20,000 zitakuwa zimetolewa kwa lengo la kuongeza usalama wa milki za ardhi