Katibu Mkuu Wizara ya UTUMISHI , Mhe.Juma Selemani Mkomi, ameipongeza taasisi ya Watumishi Housing Investments (WHI) kwa ujenzi wa nyumba zenye ubora na unaoendana na mahitaji ya watanzania, ambapo aliweka wazi kua nia ya Wizara hiyo kwa sasa ni kuhakikisha watumishi wanaendelea kupata makazi bora kupitia WHI.
Mhe. Mkomi ameyasema hayo leo Aprili 13, 2023 alipotembelea na kukagua mradi wa Nyumba za makazi ambazo zimejengwa na zinazoendelea kujengwa na Watumishi Housing Investments zilizopo katika eneo la Njedengwa Mkoani Dodoma.
Aidha Mkomi amesisitiza juu ya kuhakikisha ujenzi wa nyumba unaendelea kuzingatia ubora kama ambavyo nyumba zilizo kamilika zinavyoonekana.
“Hakikisheni mnaweka mpango mkakati kuhakikisha wilaya mpya zinapata nyumba kwaajili ya watumishi wanaokwenda kuhudumia Wananchi maeneo mbalimbali ya nchi yetu” alisema Mhe. Juma Mkomi
Pamoja na hayo Mhe. Mkomi ameipongeza taasisi ya Watumishi Housing Investments (WHI) kwa kuanzisha Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (FAIDA FUND) wenye lengo la kuinua na kukuza vipato vya watanzania wenye vipato tofauti tofauti.
Mhe. Mkomi ameiagiza WHI kuhakikisha Mfuko huo unatangazwa na fursa ya uwekezaji inawafikia watanzania wengi zaidi wakiwemo watumishi wa umma kwani kupitia kufanya uwekezaji katika mfuko huo watu wanaweza kujiongezea kipato.