Na WAF, Bungeni, Jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel amebainisha sababu zinazopelekea upotevu wa fedha katika vituo vya kutolea huduma za afya kutoka kwa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) nchini.
Dkt. Mollel amesema, Baadhi ya watoa huduma za afya wamekuwa wakiwasilisha madai yenye udanganyifu katika utoaji wa huduma kwa lengo la kujiongezea kipato kwa njia isiyo halali jambo ambalo limekuwa likisababisha kufa kwa mfuko huo.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Aprili 13, 2023 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Jesca Jonathan Msambatavangu katika Mkutano wa 11 kikao cha sita.
Ameendelea kusema, baadhi ya watoa huduma kutozingatia kwa miongozo ya tiba nchini (STG) inayotolewa na Wizara ya Afya, kama makubaliano baina ya pande zote yanavyoelekeza.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Sababu nyingine ni, kutozingatiwa kwa bei zilizoainishwa katika Mkataba wa Huduma baina ya Mfuko (NHIF) na Watoa Huduma.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema, Rais Samia amehakikisha mikoa yote nchini inahuduma za CT-SCAN, huku zikiwepo nyingine za ziada tayari kwa kuendelea kuwahudumia wananchi katika Mikoa yote nchini.
Pamoja na hayo, Dkt. Mollel amemwelekeza Mkurugenzi wa Bima ya Afya kuhakikisha ndani ya saa 24 watu wote wenye vigezo vya kupata huduma waanze kupata huduma hizo za CT-SCAN.
Kwa upande mwingine Dkt. Mollel amesema, Serikali itaendelea kuhakikisha huduma za chanjo zinaendelea kuboreka na tayari imetenga baadhi ya magari yatayotumika katika kuhakikisha huduma za chanjo zinapatikana katika maeneo yote nchini.