Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa watoto katika malezi bora ili kupunguza wimbi la watoto wa mtaani pamoja na kuzuia mmomonyoko wa maadili.
Ameyasema hayo jana usiku baada ya kufuturisha waumini wa Dini ya Kiislam nyumbani kwake Ikulu ndogo Mkoani Shinyanga,ambapo hafla hiyo ilihudhuriwa ni viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa Chama cha mapinduzi CCM, viongozi wa Dini ya Kikristo, wadau mbalimbali na baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga.
RC Mndeme amewaomba viongozi wa Dini kushirikiana pamoja katika kutokomeza mmomonyoko wa maadili ambao husababisha watoto kujiingiza kwenye uhalifu huku akisisitiza wazazi na walezi kuwalinda watoto wao ili wakue katika maadili mema.
Amewaomba viongozi wa Dini kukemea suala la mmomonyoko wa maadili linalopelekea baadhi ya vijana katika Mkoa wa Shinyanga kuiga mila na desturi za kigeni ambapo RC Mndeme ametumia nafasi hiyo kuwasihi vijana kufanya kazi halali kwa kuzingatia misingi na taratibu wa Taifa hili la Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amewaomba viongozi wa Dini kuendelea kuomba Amani, umoja na mshikamano uendelee katika Taifa hili ikiwa ni pamoja na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali ya awamu ya sita.
Amesema serikali ya Mkoa wa Shinyanga itaendelea kutoa ushirikiano katika nyanja na sekta zote katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo changamoto za kiimani na zisizo za kiiamani huku akiomba ushirikiano ili kuendeleza Amani ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Mndeme amewashukuru viongozi wa Dini kwa dua na sala ambapo amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamani kazi kubwa zinazofanywa na viongozi wa Dini katika kuimarisha Amani Nchini.
“Viongozi wa dini mmekuwa na mchango mkubwa sana kwa Taifa letu katika Nyanja mbalimbali ikiwamo Sekta ya Afya na Elimu, sababu Taasisi zenu mmekuwa mkimiliki shule na huduma za afya pamoja na kudumisha amani, na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamani mchango wenu na itaendelea kushirikiana na ninyi siku zote,”amesema RC Mndeme.
Aidha RC Mndeme amewaomba viongozi wa Dini kuendelea kuwaombea watu watu huku akiisihi jamii kuwa na utamaduni wa majitoleo kwa watu wenye uhitaji wakiwemo watu wenye ulemavu wa ngozi, wasioona pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kwamba hali hiyo itasaidia kutimiza ndoto zao.
Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga Ismail Makusanya amemshukuru na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa kuguswa kufuturisha ambapo ametumia nafasi hiyo kumumbea dua pamoja na viongozi wengine akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Kitendo alichokifanya Mkuu Mkoa kwa kufuturisha waumini wa dini ya kiislamu ni kikubwa dhawabu yake atalipwa na Mwenyezi Mungu na atamzidishia zaidi ya alichotoa.Sisi viongozi wa dini tutaendelea kuliombea amani Taifa, pamoja na kumuombea na Afya njema Mheshimiwa Rais Samia na Serikali yake yote ili aendelee kuliongoza vyema Taifa na kuwaletea maendeleo Watanzania”,
“Sisi tutaendelea kuomba Amani ya Taifa, pamoja na kumuombea Afya njema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia na Serikali yake yote kikiwamo na Chama cha Mapinduzi CCM, ili aendelee kuliongoza vyema Taifa na kuwaletea maendeleo watanzania”. amesema Sheikh Makusanya.