Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema fursa iliyopo sasa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kuunda Mfumo wa Haki Jinai, ili kujenga ufanisi katika utendaji.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo huko Ofisini kwake Migombani, Mkoa wa Mjini-Magharibi Unguja, alipokutana na kutoa maoni yake mbele ya Tume ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Maboresho ya Taasisi za Haki Jinai.
Amesema kuwa fursa hiyo ipo sasa kufuatia hatua ya kuundwa kwa Chombo muhimu cha uratibu ambacho ni hiyo Tume ya Rais ya Maboresho ya Taasisi za Haki Jinai Nchini.
Amefahamisha akisema kuwa kwa mujibu wa uoni wake ukweli utabaki kwamba ndani ya Tanzania zipo tu Taasisi zinazohusiana na kinachoitwa Haki, na baadhi yao zikiwepo bila kujitambua, bali kwa udhati Mfumo wa Haki Jinai Nchini haupo.
“Kinachokosekana pia ni pamoja na ‘criminal justice policy’ sera ya haki jinai licha ya kuwepo baadhi ya mapendekezo hapo awali ili kuleta ufanisi”, amefahamisha Mheshimiwa Othman.
Aidha Mheshimiwa Othman ameendelea kufahamisha kwa kusema, “najua tuna taasisi; najua tuna personnel; najua tuna Sheria, lakini kiukweli mfumo hasa wa haki jinai siuoni”.
Mheshimiwa Othman ambaye ametumia uzoefu wake wa Miaka 9 akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu; Miaka 9 pia akiwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), na hatimaye Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, kabla ya kuondolewa na kisha kurudi tena kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameelekeza ushauri wake katika mageuzi ya maeneo mbali mbali yanayonasibishwa na haki nchini, ambayo ni pamoja na Ukuzaji wa Raslimali, Stadi, Hadhi, Viwango, na Kuzijengea Uwezo Sekta za Haki kwa kuzingatia uwiano, huku akitaja mifumo ya Jeshi la Polisi, Upelelezi na Idara za Uendeshaji Mashtaka ambazo mifumo yake haikuzingatia ufanisi, uwezo na weledi, zaidi ya kutumikia uzalendo wa kisiasa.
Ametolea mfano utendaji wa Jeshi la Polisi hasa nyakati za chaguzi na mazingira ya kisiasa kwamba ni kigezo tosha cha udhaifu wa ukosefu wa Mfumo Haki Jinai Tanzania, kutokana na kutumikia maagizo ya kisiasa upande mmoja, kwa gharama yeyote hata iwapo ni kutenda dhulma kwa umma wa wananchi.
Mheshimiwa Othman ametolea mfano akisema, “mathalan katika hitajio pia ni pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zikiwemo Polisi, kupitia ‘recruitment’ mafunzo ambako hapakuzingatiwa ‘merit’ uwezo na vigezo hata kidogo, na ni eneo muhimu kwa maslani ya nchi.
Pia ameeleza haja ya kuwepo upelelezi wa kitaalamu wa makosa ya jinai ‘forensic criminal investigation’ akishauri kwamba ni vyema kwa mamlaka zikiwemo Maabara, Mkemia Mkuu na Uchunguzi wa Madaktari, ziende kisasa ili kujenga haiba, viwango, na hadhi ya kuaminika kitaifa na kimataifa, hasa inapohitajika kusaidia ushahidi.
Akitaja tatizo sugu la ubadhirifu, ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya ofisi, Mheshimiwa Othman amelalamikia kwa kusema, “mfumo uliopo sasa unashindwa hata kuripoti makosa makubwa na jinai inayotekelezwa na wakubwa, na hivyo inakuwa vigumu kubainisha ni nani muhalifu na yupi asiyekuwa muhalifu katika Nchi”.
“Bila ya kuondosha hili la ‘abuse of office’ mimi nasema safari haitokuwa rahisi, mengine yote tusahau kwani hao wadogo nao watachukua ‘advantage’ kwa kila mmoja kufanya anavyotaka”.
“Tunayo kazi kubwa ya kuuunda Mfumo wa Haki Jinai iwapo tuna lengo la kuleta ufanisi wa kweli’, ameeleza Mheshimiwa Othman.
Pamoja na maoni hayo, Mheshimiwa Othman ameipongeza Tume hiyo inayowajumuisha watu aliowaita ‘vigogo’ weledi sambamba na kuwatakia mafanikio mema katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akiwasilisha Ripoti fupi ya Utekelezaji tangu kuundwa kwake, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Msaafu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, amesema wamelenga kuzimulika Taasisi mbali mbali zenye mnasaba wa haki ambazo ni Jeshi la Polisi; Ofisi ya Taifa ya Mashtaka; Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Rushwa sambamba na ile ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya; pamoja na zile zinazohusika moja kwa moja zikiwemo Mahakama, Mkemia Mkuu wa Serikali, na Ustawi wa Jamii.
Amesema tayari tangu Februari 1 hadi Aprili 6, 2023 Tume imeweza kuwakabili Wakuu wa Taasisi hizo pamoja na Wananchi kupitia mbinu tofauti za Dodoso, Mikutano ya Hadhara, na Vipeperushi.
Jaji Mstaafu Chande amefafanua kwamba hadi sasa Tume hiyo imeshatembelea Vituo vya Polisi 46; Magereza 19; Imefanikisha Mikutano ya Hadhara 25; Imewahoji Wananchi 8550, katika Wilaya 50 ndani ya Mikoa ipatayo 18 Tanzania.
Amefahamisha kuwa nia yao ya kuja Zanzibar ni kujifunza na kuendeleza mahojiano kwa makundi tofauti ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba ili kupata ushauri kutoka kwa wananchi na viongozi, juu ya Mfumo wa Taasisi ya Haki Jinai.
Waliojumuika katika Ujumbe huo ni pamoja na Maafande Wastaafu, IGP Said Mwema na Ernest Mangu na Bi Saada Ibrahim Makungu; Dr. Edward Hoseah na Dr. Yahya Khamis Hamad; Balozi Ombeni Sefue, Bw. Reuben Samwel Shesha, Bw. Omari Issa na Bw. Laurean Ndumbaro (Katibu wa Kamati).